Friday, April 12, 2013

VIONGOZI UWT WATEMBELEA BURUNDI





 Picha mbalimbali za viongozi wa Umoja wa wanawake wa CCM mkoa Kigoma walipofanya ziara katika mkoa wa Ruyigi nchini Burundi kutembelea shughuli za chama cha CNDD - FDD cha nchini Burundi.(Picha na Fadhili Abdallah)



Na Fadhili Abdallah,
Ruyigi Burundi


UJUMBE wa viongozi wa watano wa jumuia ya umoja wa wanawake wa CCM (UWT) umefanya ziara ya ujirani mwema nchini Burundi na kutoa mwito kwa viongozi na wanachama wa jumuia ya wanawake wa chama tawala nchini humo CNDD – FDD  A’bakenyera Rugamba kutokubali amani ya nchi ichezewe na kuifanya nchi hiyo kurudi vitani.


Akizungumza katika mkutano wa pamoja kati ya UWT na A’bakenyera Rugamba Mjumbe wa baraza kuu Taifa la UWT, Josephine amesema kuwa wanawake wanayo nafasi kubwa katika kuhakikisha kwamba wanasimamia amani inadumishwa nchini humo.


Alisema kuwa kuvurugika kwa amani kunaathari kubwa kwa wanawake na watoto na uzoefu huo umejionyesha katika vuta ya wenyewe kwa wenyewe iliyomalizika nchini humo ambapo wanawake na watoto walikuwa wahanga wakubwa wa vita.


Akizungumzia ushirikiano na mahusiano kati ya jumuia hizo mbili Josephine ambaye ni Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Uvinza alisema kuwa mkutano huo bado na kubadilisha mawazo lakini pia unalenga kuwapa mbinu na mkakati viongozi wa jumuia hiyo kuifanya CNDD – FDD kuongoza nchi ya Burundi kwa muda mrefu.


Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Taifa wa  jumujia ya wanawake wa chama cha CNDD – FDD A’bakenyera Rugamba, Yamuremiye Goreth alisema kuwa ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao kwani katika mkutano na majadiliano ya pamoja waliyofanya yamewapa uzoefu wa nini cha kufanya katika siku zijazo.


Alisema kuwa moja ya mambo ambayo yamewapa mwanga namna ya kufanya ukiacha suala la mambo ya kisiasa alisema kuwa hata suala la uchumi linapaswa kuingizwa kwenye siasa kwa wanachama wa chama hicho kupewa nguvu za kiuchumi kwa kuanzishiwa miradi ya kujitegemea ya kuwaingizia kipato.


Naye Mwenyekiti wa Chama cha CNDD – FDD mkoa Ruyigi, Ngerageze Egide alisema kuwa chama hicho kimeweza kuongoza kwa amani hadi sasa baada ya Raisi Nkurunzinza kushika madaraka inatokana na kiongozi huyo kuondoa ubaguzi katika kuunda serikali.


Egide alisema kuwa serikali ya Burundi kwa sasa inaongozwa kwa mseto wa makabila yote kujumlishwa kwenye serikali jambo ambalo limewafanya wananchi kulifurahia lakini pia Raisi Nkurunzinza amejitahidi kutumia rasilimali za nchi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayowagusa wananchi moja kwa moja.


Mkutano huo wa pamoja wa vyama hivyo ulifikia maazimio ya kuwa na safari  za kila mwaka kwa viongozi wa jumuia hizo za wanawake za CNDD – FDD na CCM kutembeleana na kubadilisha uzoefu   katika masuala ya siasa, uchumi na utamaduni.


mwisho


WATU 50 raia wa Burundi ambao waliathirika na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi wame wameanzishiwa miradi ya kiuchumi ambayo itawasaidia kuwaingizia kipato kwa ajili ya kuendeshea maisha yao.



Katibu Mtendaji wa jumuia ya wanawake wa chama cha CNDD - FDD (A’bakenyera Rugamba), Yamuremiye Goreth alisema hayoi wakati Akitoa taarifa kwa viongozi wa jumuia ya wanawake wa CCM (UWT) mkoa Kigoma waliofanya ziara ya Ujirani mwema nchini Burundi.


Alisema kuwa sehemu ya wananchi hao walikuwa askari wakati wa vita, wapo wanawake waliofiwa na waume zao ambao walikuwa wapiganaji na wazee ambao familia zao ziliteketea kwenye vita hiyo.


Goreth alisema kuwa watu hao wamepatiwa eneo la Hekta 14 ambalo wamepanda mazao mchanganyiko ikiwemo Mananasi, Mihogo na ndizi katika eneo la kijiji cha Nyaburondwe, tarafa ya Butaganzwa mkoa wa Ruyigi.


katika uwezeshaji huo Raisi Pierre Nkurunzinza amekipatia kikundi hicho kiasi cha Faranga milioni 6.5 sawa na zaidi ya shilingi milioni saba za Tanzania kwa ajili ya kupatiwa utaalam wa kilimo na uimarishaji wa kikundi chao.


Katibu huyo Mtendaji wa A’bakenyera Rugamba alisema kuwa serikali imechukua hatua hiyo ili kuwasaidia watu hao kutokana na athari za kijamii na kiuchumi walizopata ambazo zimepelekea kuathirika kisaikolojia.


Wakizungumzia hatua viongozi wa UWT waliokuwa kwenye ziara hiyo waliishukuru serikali ya Burundi inayoongozwa na Raisi Nkurunzinza kwa kuchukua hatua mbalimbali za kurekebisha maisha wa watu nchini humo.


Mjumbe wa baraza kuu la UWT Taifa, Josephine Hosea alisema kuwa jumuia hiyo iko pamoja na chama hicho na serikali kwa jumla katika kusaidia kwa hali na mali kuona wananchi wa Burundi wanarudia maisha yao ya kawaida ya kabla ya vita.


mwisho.

No comments:

Post a Comment