Friday, April 5, 2013

BILIONI 32 KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI KIGOMA UJIJI




Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MAMLAKA ya maji safi na maji taka Kigoma Ujiji (KUWASA) inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 32 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za maji katika manispaa ya kigoma Ujiji na vitongoji vyake.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa maji wa manispaa ya kigoma Ujiji kwa ajili ya kutambulisha mradi huo Msimamizi wa mradi huo, Alex Kaaya kutoka wizara ya maji na umwagiliaji amesema kuwa mradi huo unapaswa kukamilika mwezi Machi mwaka 2015.

Kaaya amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kutokana na ruzuku iliyotolewa na jumuia ya ulaya  na Shirika la KFW la Ujerumani kwamba kutokana na kutolewa kwa fedha zote za mradi wanatarajia mradi utakamilika katika muda uliopangwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka ya maji safi na maji taka Kigoma Ujiji, Simon Rutuga amesema kuwa sehemu kubwa ya utekelezaji wa mradi itajikita katika kuanzisha chanzo kipya, ujenzi wa matanki ya kuhifadhia maji na usambazaji wa mtandao mpya wa maji kwa urefu wa kilometa 70 kuhakikisha maji yanafika kwa wananchi.

Rutuga alisema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kunalenga pamoja na kuboresha huduma za maji katika manispaa hiyo lakini pia kuifanya mamlaka hiyo iwe na uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 100 na hilo litawezekana kwa wananchi kulipia bili zao kwa wakati kulingana na kuridhika na huduma wanayopata.

Akifungua mkutano huo Mkuu wa wilaya Kigoma, Ramadhani Maneno amewataka wanasiasa kusaidia kuweka utashi wao katika kuufanya mradi kukamilika kwa wakati badala ya kuingilia na kukwamisha utekelezaji wa mradi.

Maneno alisema kuwa hivi sasa wananchi wamekuwa wakipiga kelele sana kutokana na kushsngazwa kuona ziwa likiwa mita chache kutoka kwenye makazi yao lakini huduma za maji zimekuwa na matatizo makubwa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment