Friday, April 12, 2013

JAMBAZI SUGU MBARONI NA SHEHENA YA RISASI

                               Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Fraiser Kashai


                                             Na Fadhili Abdallah,Kigoma
 
JESHI la polisi mkoani Kigoma limemtia mbaroni mwenyekiti wa kijiji cha Kwaga wilaya ya Kasulu mkoani hapa akihusishwa na uchochezi uliopelekea mauaji ya mwananchi mmoja wa kijiji hicho.

Kamanda wa polisi Mkoa kigoma, Fraiser Kashai alisema kuwa mwenyekiti huyo, Baraka Christopher anahusishwa kuwashawishi wananhi wa kijiji hicho kuvamia makazi ya Peter Lukaya ambapo walichoma moto nyumbani yake na kumuua wakimuhusisha na kufanya vitendo vya kishirikina.

Sambamba na mwenyekiti huyo Kamanda Kashai alisema kuwa pia polisi inawashikilia wananchi wengine wawili, Ramadhani Mohamed na Revocatus Mpomongo wakihusishwa na mauaji hayo.

Aidha baada ya mauaji hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita polisi wilaya ya Kasulu ilianza kuendesha msako kijiji hapo kuwatafuta watuhumiwa wa mauaji hayo hali iliyozua mtafaruku mzito kijijini hapo.

Wakati polisi wakiendesha msako wa kuwatafuta wauaji wananchi wa kijiji hicho walilalamikia vitendo vilivyokuwa vikifanywa na polisi ambapo wananchi hao walifanya maandamano kupinga unyanyasaji wa polisi katika kamata kamata hiyo.

Mwandishi wa habari hii alishuhudia wananchi waliozuia barabara ya Kigoma kwenda Kasulu kwa kujaza mawe barabarani hali iliyolazimu polisi kutumia silaha za moto na mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya watu hao.

Wakiongea na gazeti hili baadhi ya wananchi wa kijiji hicho ambao walihofia kutajwa majina yao waliwashutumu polisi waliokuwa wakifanya msako wa kuwatafuta watuhumiwa kwa kusema kuwa polisi hao walikuwa wakivamia makazi ya watuhumiwa na kupora mali.

Mmoja wa watuhumiwa aliyetajwa kuhusika na kadhia hiyo ni mwalim, Grace Kingaru ambaye katika msako huo alipoteza simu mbili na pesa kiasi cha shilingi 300,000 na baadaye simu yake moja ilikamatwa ikiwa imetuma meseji ya matusi kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa kigoma.

Mwalim huyo alikamatwa akituhumiwa kuhusika na kuchochea wananchi kufanya vurugu kupinga vitendo vya unyanyasaji wa polisi vilivyopelekea uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali ambapo hivi sasa mwalim huyo yuko nje kwa dhamana.

Kamanda wa polisi Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai alisema kuwa si haki kwa wananchi kufanya vurugu na kuharibu mali badala yake wanapaswa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kama kuna vitendo kama hivyo.

Alisema kamanda Kashai kuwa Mwenyekiti huyo wa kijiji na watu wengine wawili ambao walikamatwa kuhusika na mauaji hayo wanatarajia kufikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi utakapokamilika.

Mwisho.

MTU mmoja ambaye anasadikiwa kuwa ni jambazi sugu amekamatwa na polisi akiwa na risasi 1200 sa bunduki za SMG,G3 na SAR akiwa katika harakati za kuzisafirisha risasi hizo kwenda kuziuza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma jana Kamanda wa polisi Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai alimtaja mtu huyo kwamba Mwanzo Wilson aliyejitambulisha kuwa ni mkulima na mkazi wa kijiji cha Kitambuka wilaya ya Buhigwe mkoani hapa mpakani na nchi jirani ya Burundi.

Kamanda Kashai alisema kuwa kukamatwa kwa mtu huyo kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwepo kwa mpango wa mtu huyo kuzisafirisha risasi hizo katika mbinu ambayo ingewahadaa vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kumkamata.

 Ili kukwepa vizuizi vya vyombo vya ulinzi na usalama Kamanda Kashai alisema kuwa mtuhumiwa huyo alizificha risasi hizo katika dumu la mafuta ya maweze jambo ambalo lingekuwa taabu kwa polisi kumtilia mashaka.

Baadhi ya askari kituoni hapo waliweza kuwaonyesha waandishiwa habari picha mbalimbali za miaka ya nyuma zikimuonyesha mtuhumiwa akiwa amekamatwa kwa tuhuma za ujambazi na moja ya matukio yake ni wizi uliotokea katika benki moja jijini Dar es Salaam miaka mitatu iliyopita.

Aidha katika tukio lingine polisi inamtafuta Tanu Nyandila Mkulima na mkazi wa kijiji cha Kagerankanda wilaya Kasulu baada ya kukimbia na kutelekeza bunduki mbili aina ya gobore ambazo alikuwa akizitumia kwenye matukio ya uhalifu na uwindaji haramu.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa polisi kwa kushirikiana na askari wa idara ya wanyama pori wa pori la hifadhi la Muyowosi Kigosi walipata habari za kuwepo kwa mtuhumiwa huyo hata hivyo kabla ya kumtia mbaroni mtuhumiwa alikimbia na kutelekeza magobore hayo mawili.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment