Friday, April 5, 2013

JAMBAZI SUGU MBARONI NA SHEHENA YA RISASI




MTU mmoja ambaye anasadikiwa kuwa ni jambazi sugu amekamatwa na polisi akiwa na risasi 1200 sa bunduki za SMG,G3 na SAR akiwa katika harakati za kuzisafirisha risasi hizo kwenda kuziuza.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma jana Kamanda wa polisi Mkoa Kigoma, Fraiser Kashai alimtaja mtu huyo kwamba Mwanzo Wilson aliyejitambulisha kuwa ni mkulima na mkazi wa kijiji cha Kitambuka wilaya ya Buhigwe mkoani hapa mpakani na nchi jirani ya Burundi.

Kamanda Kashai alisema kuwa kukamatwa kwa mtu huyo kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwepo kwa mpango wa mtu huyo kuzisafirisha risasi hizo katika mbinu ambayo ingewahadaa vyombo vya ulinzi na usalama kuweza kumkamata.

 Ili kukwepa vizuizi vya vyombo vya ulinzi na usalama Kamanda Kashai alisema kuwa mtuhumiwa huyo alizificha risasi hizo katika dumu la mafuta ya maweze jambo ambalo lingekuwa taabu kwa polisi kumtilia mashaka.

Baadhi ya askari kituoni hapo waliweza kuwaonyesha waandishiwa habari picha mbalimbali za miaka ya nyuma zikimuonyesha mtuhumiwa akiwa amekamatwa kwa tuhuma za ujambazi na moja ya matukio yake ni wizi uliotokea katika benki moja jijini Dar es Salaam miaka mitatu iliyopita.

Aidha katika tukio lingine polisi inamtafuta Tanu Nyandila Mkulima na mkazi wa kijiji cha Kagerankanda wilaya Kasulu baada ya kukimbia na kutelekeza bunduki mbili aina ya gobore ambazo alikuwa akizitumia kwenye matukio ya uhalifu na uwindaji haramu.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa polisi kwa kushirikiana na askari wa idara ya wanyama pori wa pori la hifadhi la Muyowosi Kigosi walipata habari za kuwepo kwa mtuhumiwa huyo hata hivyo kabla ya kumtia mbaroni mtuhumiwa alikimbia na kutelekeza magobore hayo mawili.

Mwisho.
 Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraiser Kashai (kushoto) akionyesha kwa waandishi wa habari bunduki aina ya Gobore ambayo ilikamatwa katika msako wa polisi sambamba na risasi 1200  (Picha na Fadhili Abdallah)

No comments:

Post a Comment