Thursday, December 20, 2012

WAWILI WAUAWA KWA WIZI WA MBUZI


                                             Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WATU wawili wakazi wa kijiji Nyamtukuza wilaya ya kibondo mkoani Kigoma wameuawa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali wakituhumiwa kuiba mbuzi wawili wenye thamani ya shilingi 40,000.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraiser Kashai aliwataja watu hao waliouawa kuwa ni Nongo Bufinkri (36) na Azimio Muhabwa ambao waliiba mbuzi mali ya Sibalina John na waliuawa juzi majira ya mchana kijiji hapo.

Hata hivyo Kamanda Kashai alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambapo mtuhumiwa mmoja alifanikiwa kukimbia kabla ya wenzake kukutwa na mauti.

Katika tukio lingine kamanda huyo wa polisi mkoa kigoma alisema kuwa mkulima mmoja mkazi wa kijiji cha Kazuramimba Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Stephano Muhunzi (70) aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni mjambazi.

Alisema kuwa katika tukio hilo watu watano walivamiwa nyumbani kwa marehemu majira ya mchana na baada ya kumjeruhi vibaya mwilini waliondoka na kondoo sita wenye thamani ya shilingi 300,000.

Aidha hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye amekamatwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo na kwamba juhudi za kuwatafuta wauaji zinaendelea.

Katika hatua nyingine Kamanda wa polisi mkoa kigoma, Fraiser Kashai amewataka wananchi mkoani Kigoma kujihadhari na watu wasiowema amabo wanafika kwenye makazi yao na kuwataka kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapohisi kuna kitu cha namna hiyo.

Pia kamanda huyo wa polisi mkoa kigoma amesema kuwa jeshi lake limejipanga vizuri kuhakikisha kwamba kuna na amani na usalama wakati wote wa kipindi cha sikukuu za Christmas na mwaka mpya.

Mwisho.


RUN WAY AIRPORT KIGOMA

sehemu ya uwanja wa ndege Kigoma ambayo hivi sasa iko chini ya matengenezo kwa ajili ya kuifanya njia hiyo ya kurukia ndege kuwa ya kiwango cha lami

UKAGUZI UWANJA WA NDEGE KIGOMA

Waziri wa uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe katikati akitembelea na kukagua matengenezo ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami katika uwanja wa ndege wa Kigoma (wa kwa kulia) ni Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini, Dk.Agnes Kijazi.


Na Mwajabu Kigaza,Kigoma

WAZIRI wa uchukuzi Harison Mwakyembe ameitaka mamlaka ya viwanja vya ndege nchini kuhakikisha wananchi wa manispaa ya Kigoma ambao wanatakiwa kuhama kupishwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma wanalipwa katika kipindi kifupi kijacho.

Akizungumza muda mfupi baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa uwanja huo ambao unahusisha matengenezo ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami  Mwakyembe alisema kuwa hataki kusikia suala la fidia linakwamisha awamu ya pili ya upanuzi wa uwanja huo.

Akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa idara mbalimbali katika uwanja wa ndege wa Kigoma Waziri Mwakyembe alisema kuwa ni lazima hadi kufikia mwezi Februari mwaka ujao wakazi hao wawe wameshalipwa na mwezi Julai awamu ya pili ya uwanja huo iweze kuanza

Katika awamu ya kwanza ya mradi huo inahusisha ujenzi wa mita 1800 ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami huku awamu ya pili ikihusisha kuendeleza urefu huo na kufikia mita 3100 ambazo zitawezesha ndege aina ya Boing 737 na air Bus kutua sambamba na ujenzi wa majengo mbalimbali uwanjani hapo ikiwemo jengo la kisasa la abiria.

Aidha pamoja na hatua nyingine Waziri huyo amesema kuwa ameridhishwa na kazi ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa kigoma inayofanywa na kampuni ya Syno Hydro ya China ambapo ameitaka kampuni kuhakikisha kwamba uwanja huo unafunguliwa katika kipindi kifupi kijacho ili kutoa nafuu ya usafiri wa ndege kwa wakazi wa mikoa ya Magharibi.

Alikusema kuwa kampuni hiyo imejenga imani  kubwa kwa serikali katika kuhakikisha inapewa  awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa uwanja huo kufikia hadhi ya uwanja wa ndege  wa kimataifa.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo mhandisi mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya stewart Scot International  ya Afrika Kusini , Cleopa Mpembeni amesema kuwa kumekuwa na maendeleo mazuri ya mradi huo katika awamu hii ya kwanza  na kwamba matarajio na kuhakikisha ujenzi huo unaisha kufikia mwezi Februari mwaka ujao.

Mpembeni alisema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili kwwa sasa ni kunyesha kwa mvua nyingi mkoani kigoma jambo ambalo limesababisha wakati mwingine kusimamisha kazi kwa siku  nzima au kufanya kazi hiyo nyakati za usiku.

Mwisho.

KUTUNUKU VYETI CHUO CHA HALI YA HEWA KIGOMA

Waziri wa uchukuzi Harison Mwakyembe (wa pili kushoto) akitunuku  cheti kwa amina Hussein (kulia) mmoja wa wahitimu 28 wa Diploma ya hali ya hewa wakati wa mahafali ya chuo cha hali ya hewa mjini Kigoma kwa mwaka huu 2012    (picha na Fadhili Abdallah)


Waziri wa uchukuzi Harison Mwakyembe  ameiagiza mamlaka ya hali ya hewa nchini( TMA) kufanya utafiti na kuon namna gani wanaweza kuwasaidia wananchi kukabiliana radi zinazotokea na kuwadhulu watu wengi nchini kila siku.


Akizungumza katika mahafali ya kuwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya diploma ya hali ya hewa katika chuo cha hali ya hewa kigoma Mwakyembe alisema kuwa n lazima wahitimu waonyeshe umahiri wao katika kuwasaidia wananchi kutokana na taaluma wanayopata.


Aalisema kuwa idara ya hali ya hewa imekuwa na umuhimu mkubwa kwa maisha ya wananchi lakini umuhimu huo usiishie kwenye utabiri tu lazima wasomi wanaohitimu mafunzo katika vyuo vya hali ya hewa ndani na nje ya nchi kuwasaidia wananchi kuona namna gani tenkolojia ya kukabiliana na radi inaweza kuwasaidia wananchi.


Aidha sambamba na hilo waziri huyo wa uchukuzi alisema kuwa mamlaka haina budi kurahisisha utabiri wa hali ya hewa na kuufanya uwe na manufaa ya moja kwa moja kwa mwananchi ili jamii na taifa liweze kupanga mipango yake kwa kuzingatia utabiri unaotolewa na idara hiyo.


Waziri Mwakyembe alisema kuwa ili kwenda na wakati na wananchi waone umuhimu wa uwepo wa taasisi hiyo  ni budi TMA  ianze kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa maeneo madogo pamoja na elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa.


kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini,Dk.A gnes kijazi amesema katika kuboresha shughuli za mamlaka , wako katika hatua za mwisho kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Dar es salaam kuanza kutoa shahada ya hali ya hewa.


Dk.Kijazi alisema kuwa hata hivyo ufinyu wa bajeti umekuwa ukikwaza utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kimaendeleo ya mamlka hiyo na kwamba kwa mwaka ujao serikali imeahidi kuiongeza bajeti mamlaka hiyo ili iweze kutekeleza mipango yake kwa manufaa ya nchi.


kwa upande wao wahitimu wa mafunzo hayo , pamoja na kuelezea matumaini yao baada ya kumaliza masomo , wameiomba serikali kuyapatia ufumbuzi matatizo ya maabara, vitabu, majengo na usafiri yanayokikabili chuo hicho pekee cha hali ya hewa nchini.


Mmoja wa wahitimu hao, Shaban Dilunga  akisoma risala kwa niaba ya wajitimu hao alisema kuwa pamoja na changamoto hizo lakini ufinyu wa bajeti na uchache wa fedha wanazipowa umechangia kuwafanya washindwe kufanya mafunzo kwa vitendo (Field na study tour).


mwisho

KUHITIMU MAFUNZO YA MGAMBO




MKUU wa mkoa Kigoma Issa Machibya amewataka wahitimu wa kozi ya mgambo kuzingatia nidhamu na kutumia mafunzo hayo kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii badala ya kuwa chanzo cha kuwaingiza kwenye vitendo vya kihalifu.

Machibya alisema hayo katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma, Ramadhani Maneno wakati wa kufunga mafunzo ya mgambo kwa watumishi 168 wa serikali mkoani Kigoma yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa serikali ya mkoa imeamua kufanyika kwa mafunzo hayo lengo likiwa kuwajengea ukakamavu watumishi wake lakini pia kuongeza uzalendo miongoni mwa watumishi wake hasa vijan ambao wameanza kazi miaka ya hivi karibuni.

Awali katika risala ya wahitimu hao iliyosomwa kwa niaba yao na Noel Byamungu wamesema kuwa kumekuwa wamekuwambana na changamoto mbalimbali katika mafunzo hayo ikiwemo kitendo cha mwajiri kushindwa kuwalipa stahili zao kwa wakati.

Byamungu alisema kuwa kitendo kimechangia  kuwafanya washiriki kutoshiriki mafunzo kwa uhuru lakini kwani kimekuwa kikiharibu bajeti zao ambapo wameahidi kwamba watatumia mafunzo hayo kwa kadri ya kiapo walichokula kwa maslahi ya Watanzania wote.

Mwisho.

MSAADA WA BAISKELI KWA WATOA HUDUMA MAUMBANI

Mkuu wa wilaya Kasulu Dahn Makanga akimkabidhi baiskeli Thecla Mtereke mmoja wa watoa huduma kwa wagonjwa wa ukimwi majumbani na magonjwa sugu ili kuwawezesha watoa huduma hao kufanya kazi zao kwa urahisi anayeshuhhudia ni Sister Philipina Rubavu, Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki Kigoma



KANISA katoliki jimbo la kigoma limekabidhi baiskeli 88 zenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa watoa huduma kwa wagonjwa wa ukimwi majumbani wilayani Kasulu ili kuwawezesha kuzitumia baiskeli hizo kurahisisha mawasiliano kati yao na wagonjwa wanaowahudumia.

Baiskeli hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa wilaya kigoma, Dahn Makanga na Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki, Philipina Rubavu ambapo naye Mkuu wa wilaya Kasulu alikabidhi baiskeli hizo kwa watoa huduma 25 kwaniba ya watoa huduma wengine katika hafla iliyofanyika mjini Kasulu mwishoni mwa wiki iliyopita

Akikabidhi baiskeli hizo kwa watoa huduma Mkuu wa wilaya Kasulu, Dahn Makanga amewataka watoa huduma hao kuzitumia baiskeli hizo kuwafikia wagonjwa na kuwapatia msaada wanaohitaji.

Makanga alisema kuwa ni wazi kazi wanayofanya watoa huduma hao ni kubwa na hailingani na kiwango cha posho wanachopewa kwa kuwa wamekubali kujitoa na kwamba baiskeli hizo ziwe motisha kwao kupunguza adha kutembea umbali mrefu kuwafuata wagonjwa na kuwapatia huduma.

Naye Philipina Rubavu, Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki Kigoma alisema kuwa msaada huo umetolewa kupitia Tanzania Interfaith Partnership iliyo chini ya Tume ya Taifa ya kudhibiti ukimiw nchini (TACAIDS).

Alisema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali watoa huduma hao ambao pia wanajishughulisha na kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu wamekuwa na changamoto kubwa ya kufika maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa watoa huduma hao wanawahudhumia wagonjwa wa ukimwi wanaougulia majumbani na wagonjwa wengine zaidi ya 400 na watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi ya 1000 wakifanya kazi katika vijiji zaidi ya 25 wilayani humo.

Wakizungumzia msaada huo  baadhi ya watoa huduma hao walisema kuwa imekuwa faraja kubwa kwao kupata usafiri huo ambao utapunguza kwa kiasi changamoto ya usafiri wa kufikia maeneo mbalimbali ya utoaji huduma iliyokuwa ikiwakabili.

Thecla Mtereke na Laurian Ntamahurilo alisema kuwa kabla ya kupata baiskeli hizo walikuwa wakipata adha kubwa ya kutembea kwa mguu umbali mrefu kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa ajili ya kuwafuata wagonjwa wanaowahudhumia.

Mwisho.



Sunday, November 25, 2012

RAISI WA UTPC NDANI YA KIGOMA PRESS




Raisi wa Muungano wa vilabu vya waandishi wa habari nchini (UTPC) Keneth Simbaya (wa pili kulia) akimsindikiza Mkuu wa wilaya kigoma (wa pili Kushoto) baada ya kufungua mkutano wa wadau na kuzindua blog ya Kigoma Press Club (kushoto) ni Mwenyekiti wa KGPC Deo Nsokolo na kulia ni Katibu Tawala wa wilaya Kigoma


Raisi wa Muungano wa vilabu vya waandishi wa habari nchini Keneth Simbaya Kati kati akiwa katika ofisi za Kigoma Press Club muda mfupi baada ya kuwasili mkoani humo kuhudhuria mkutano wa wadau wa habari na mkutano mkuu maalum wa Kigoma Press Club (kushoto) ni Mwenyekiti Deo Nsokolo na (kulia) ni Mwanachama Winfrida Bwire.

Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Kigoma Deo Nsokolo (wa pili kushoto) akimueleza jambo Mkuu wa wilaya Kigoma (katikati) kuhusu blog ya chama cha waandishi wa habari mkoa Kigoma wakati wa mkutano wa wadau (wa pili kulia) ni Raisi wa muungano wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania Keneth Simbaya (Picha na Fadhili Abdalla)

WADAU KUTOKA TAASISI NA MASHIRIKA MBALIMBALI MKOANI KIGOMA WAKISHUHUDIA UZINDUZI WA BLOG YA KIGOMA PRESS CLUB

BAADA YA UZINDUZI MKUU WA WILAYA KIGOMA RAMADHANI MANENO ALIYOA NENO KWA WADAU NA WAANDISHI WA HABARI WALIOHUDHURIA MKUTANO WA WADAU MKOANI KIGOMA

Thursday, November 22, 2012

MSAADA KUTOKA WORLD LUNG FOUNDATION

 mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya akipokea msaada wa moja ya mashine tano za upasuajia zenye thamani ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya vituo vitano vya afya mkoani Kigoma kutoka kwa Brigita Steffan (Katikati) Mke wa mkurugenzi wa miradi wa shirika la World Lung Foundation Staffan Bergstrom (kulia) katika hafla ya kukabidhi mashine hiyo kwa ajili ya Kituo cha Afya Ujiji Manispaa ya Kigoma Ujiji



Mkuu wa mkoa kigoma Issa Machibya akikata utepe kuashiria kuzinduliwa kwa huduma za upasuaji katika kituo ch afya Ujiji manispaa ya Kigoma Ujiji kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika la World Lung Foundation Steffan Bergstrom.

SHIRIKA la Wolrd Lung Foundation lenye makao yake makuu nchini Marekani
limetoa msaada wa vifaa vya upasuaji kwa ajili ya  kituo cha afya cha Ujiji
manispaa ya Kigoma Ujiji ili kusiadia upasuaji kwa kina mama wajawazito
wanaoapata matatizo wakati wa kujifungua.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 100 vilikabidhiwa kwa Mkuu
wa mkoa Kigoma,Issa Machibya na Brigita Staffan mke wa Mkurugenzi wa miradi
wa shirika hilo hapa nchini, Staffan Bergstrom.

Akikabidhi wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa miradi wa
World Lung Founation nchini, Staffan Bergstrom alisema kuwa ni wazi kuanza
kutumika kwa vifaa hivyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa kina mama ambao upata
matatizo wakati wa kujifungua na wakati mwingine kufa.

Alisema kuwa shirika hilo limetoa mchango huo ikiwemo ni sehemu ya pato la
Meya wa Jiji la London, Peter Bloomber ambaye aliamua kujitolea sehemu ya
pato lake kwa ajili kusaidia matibabu ya kina wanaopata matatizo wakati wa
kujifungua.
 

Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa mkoa kigoma Issa Machibya alisema kuwa
kutolewa kwa vifaa hivyo na kutumika katika kituo hicho cya afya ujiji
kutasaidia kupunguza kama siyo kumaliza tatizo la vifo vya  kina mama
wakati wa kujifungua na itakuwa inatimiza lengo la nne la malengo ya
millennia.

Alisema kuwa ni wazi kufungwa kwa vifaa hivyo katika kituo hicho cha afya
kutapunguza msongamano katika hospitali ya Rufaa ya Maweni ambayo ilikuwa
hospitali pekee iliyokuwa ikitegemewa kwa upasuaji na wakazi wa manispaa ya
Kigoma Ujiji.

Baadhi ya kina mama waliohudhuria hafla hiyo wamesema kuwa kufungwa kwa
mashine ya upasuaji kwenye kituo hicho cha afya kutapunguza usumbufu wa
kutegemea hospitali ya maweni ambayo kwao ilikuwa ni hospitali pekee
iliyokuwa ikifanya upasuaji hapa mjini.

Mtendamema Bandora na Hamisa Kassim wakazi wa Ujiji mjini hapa walisema
kuwa kufungwa kwa mashine hizo ni mkom bozi kwao na wametoa wito kwa kina
mama wajawazito kutumia vituo vya afya kwa ajili ya kwenda kujifungulia
badala ya kujifungulia nyumbani au kwa wakunga.

Mwisho.