Thursday, December 20, 2012

UKAGUZI UWANJA WA NDEGE KIGOMA

Waziri wa uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe katikati akitembelea na kukagua matengenezo ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami katika uwanja wa ndege wa Kigoma (wa kwa kulia) ni Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini, Dk.Agnes Kijazi.


Na Mwajabu Kigaza,Kigoma

WAZIRI wa uchukuzi Harison Mwakyembe ameitaka mamlaka ya viwanja vya ndege nchini kuhakikisha wananchi wa manispaa ya Kigoma ambao wanatakiwa kuhama kupishwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma wanalipwa katika kipindi kifupi kijacho.

Akizungumza muda mfupi baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa uwanja huo ambao unahusisha matengenezo ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami  Mwakyembe alisema kuwa hataki kusikia suala la fidia linakwamisha awamu ya pili ya upanuzi wa uwanja huo.

Akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa idara mbalimbali katika uwanja wa ndege wa Kigoma Waziri Mwakyembe alisema kuwa ni lazima hadi kufikia mwezi Februari mwaka ujao wakazi hao wawe wameshalipwa na mwezi Julai awamu ya pili ya uwanja huo iweze kuanza

Katika awamu ya kwanza ya mradi huo inahusisha ujenzi wa mita 1800 ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami huku awamu ya pili ikihusisha kuendeleza urefu huo na kufikia mita 3100 ambazo zitawezesha ndege aina ya Boing 737 na air Bus kutua sambamba na ujenzi wa majengo mbalimbali uwanjani hapo ikiwemo jengo la kisasa la abiria.

Aidha pamoja na hatua nyingine Waziri huyo amesema kuwa ameridhishwa na kazi ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa kigoma inayofanywa na kampuni ya Syno Hydro ya China ambapo ameitaka kampuni kuhakikisha kwamba uwanja huo unafunguliwa katika kipindi kifupi kijacho ili kutoa nafuu ya usafiri wa ndege kwa wakazi wa mikoa ya Magharibi.

Alikusema kuwa kampuni hiyo imejenga imani  kubwa kwa serikali katika kuhakikisha inapewa  awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa uwanja huo kufikia hadhi ya uwanja wa ndege  wa kimataifa.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo mhandisi mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya stewart Scot International  ya Afrika Kusini , Cleopa Mpembeni amesema kuwa kumekuwa na maendeleo mazuri ya mradi huo katika awamu hii ya kwanza  na kwamba matarajio na kuhakikisha ujenzi huo unaisha kufikia mwezi Februari mwaka ujao.

Mpembeni alisema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili kwwa sasa ni kunyesha kwa mvua nyingi mkoani kigoma jambo ambalo limesababisha wakati mwingine kusimamisha kazi kwa siku  nzima au kufanya kazi hiyo nyakati za usiku.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment