Thursday, December 20, 2012

MSAADA WA BAISKELI KWA WATOA HUDUMA MAUMBANI

Mkuu wa wilaya Kasulu Dahn Makanga akimkabidhi baiskeli Thecla Mtereke mmoja wa watoa huduma kwa wagonjwa wa ukimwi majumbani na magonjwa sugu ili kuwawezesha watoa huduma hao kufanya kazi zao kwa urahisi anayeshuhhudia ni Sister Philipina Rubavu, Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki Kigoma



KANISA katoliki jimbo la kigoma limekabidhi baiskeli 88 zenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa watoa huduma kwa wagonjwa wa ukimwi majumbani wilayani Kasulu ili kuwawezesha kuzitumia baiskeli hizo kurahisisha mawasiliano kati yao na wagonjwa wanaowahudumia.

Baiskeli hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa wilaya kigoma, Dahn Makanga na Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki, Philipina Rubavu ambapo naye Mkuu wa wilaya Kasulu alikabidhi baiskeli hizo kwa watoa huduma 25 kwaniba ya watoa huduma wengine katika hafla iliyofanyika mjini Kasulu mwishoni mwa wiki iliyopita

Akikabidhi baiskeli hizo kwa watoa huduma Mkuu wa wilaya Kasulu, Dahn Makanga amewataka watoa huduma hao kuzitumia baiskeli hizo kuwafikia wagonjwa na kuwapatia msaada wanaohitaji.

Makanga alisema kuwa ni wazi kazi wanayofanya watoa huduma hao ni kubwa na hailingani na kiwango cha posho wanachopewa kwa kuwa wamekubali kujitoa na kwamba baiskeli hizo ziwe motisha kwao kupunguza adha kutembea umbali mrefu kuwafuata wagonjwa na kuwapatia huduma.

Naye Philipina Rubavu, Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki Kigoma alisema kuwa msaada huo umetolewa kupitia Tanzania Interfaith Partnership iliyo chini ya Tume ya Taifa ya kudhibiti ukimiw nchini (TACAIDS).

Alisema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali watoa huduma hao ambao pia wanajishughulisha na kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu wamekuwa na changamoto kubwa ya kufika maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa watoa huduma hao wanawahudhumia wagonjwa wa ukimwi wanaougulia majumbani na wagonjwa wengine zaidi ya 400 na watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi ya 1000 wakifanya kazi katika vijiji zaidi ya 25 wilayani humo.

Wakizungumzia msaada huo  baadhi ya watoa huduma hao walisema kuwa imekuwa faraja kubwa kwao kupata usafiri huo ambao utapunguza kwa kiasi changamoto ya usafiri wa kufikia maeneo mbalimbali ya utoaji huduma iliyokuwa ikiwakabili.

Thecla Mtereke na Laurian Ntamahurilo alisema kuwa kabla ya kupata baiskeli hizo walikuwa wakipata adha kubwa ya kutembea kwa mguu umbali mrefu kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa ajili ya kuwafuata wagonjwa wanaowahudhumia.

Mwisho.



No comments:

Post a Comment