Tuesday, June 3, 2014

MAZISHI YA SHIDA SALUM MAMA MZAZI WA ZITTO KABWE




 Naibu Spika wa bunge Job Ndugai (kulia) akiwa katika mazishi ya Mama yake mzazi zitto Kabwe mbunge wa jimbo la kigoma kaskazini Shida Salum yaliyofanyika mjini Kigoma (wa pili Kulia) Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma Walid Kabourou,wabunge Nimrod Mkono na Ally Kesi.


 Baadhi ya wabunge wa bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyama vya siasa wakiwa na Zitto Kabwe wakielekea makaburi ya Rubengela Mjini Kigoma kwa mazishi


   ZITTO ATOA YA MOYONI MSIBA WA MAMA YAKE


MBUNGE wa jimbo la Kigoma Kaskazini Zitto ameongoza maelfu ya viongozi na wananchi kutoka pande mbalimbali za nchi katika mazishi ya mama yake Mzazi Shida Salum na kutoa agizo kwa Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai na Mwenyekiti wa CUF Ibrahimu Lipumba kumuenzi mama yake kwa kuwaletea watanzania katiba mpya wanayoitaka.

Zitto alisema hayo nyumbani kwa Marehemu mama yake mtaa Kisangani mwanga mjini kigoma  muda mfupi kabla ya kuelekea makaburi ya Rubengela mjini Kigoma ambako mwili wa Shida Salum ulizikwa.

Mbunge huyo Kijana alisema kuwa kama kweli viongozi hao wanataka kumuenzi mama yake wamalize tofauti zao na kulifanya bunge la katiba kuendelea na shughuli yake ya kuwaletea Watanzania katiba itakayowafaa kwa muda mrefu.

Alisema kuwa Mama yake alikuwa mjumbe wa bunge hilo la katiba kufuatia kuteuliwa na Raisi Jakaya kikwete jambo ambal lingempa nafasi ya kuandika historia ya kuwa mmoja wa wajumbe wa bunge hilo katika kuandika katiba mpya ya Tanzania.

Zitto alisema kuwa hata hivyo ugonjwa uliokuwa ukimsumbua na mwenyezi mungu kumpitisha kudra zake umeondoa nafasi ya mama yake kuandika historia hiyo na kwamba kilichobaki ni kwa viongozi na wajumbe wa bunge la katiba kufikia maridhiano na kuandika katiba hiyo.

Alisema kuwa amejitahidi kwa kadri ya uwezo wake katika kuhakikisha anamsaidia mama yake kupata mataibabu ambayo yangerudisha afya yake na kumfanya arusi kwenye shughuli zake za kawaida lakini mungu alipitisha maamuzi yake ambayo hakuna wa kuyapinga.

Kwa upande wake Naibu Spika wa bunge la Tangazania,Job ndugai ambaye aliongeza wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mazishi hayo amemuelezea shida Salum kama mtu ambaye alikuwa mtetezi wa watanzania wa hali ya chini.

Hata hivyo Ndugai alisema kuwa Yaliyotokea ni mapenzi ya mungu na kuitaka familia  wasihuzunike kiasi cha kupitiliza wakae pamoja na kuweka familia pamoja na kusonga mbele katika utekelezaji wa majukumu yao ya taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha wananchi (CUF),Profesa Ibrahimu Lipumba alisema kuwa shida Salum alisimama kuwapigania watu wenye ulemavu mchango ambao alikusudia kuutoa kwenye bunge maalum la Katiba.

Hata hivyo Lipumba alionya kuwa kama kweli watu wanania ya kumuenzi marehemu shida Salum hawana budi kusikiliza maoni ya wananchi walio wengi katika kuipata katiba mpya badala ya watu wachache kutaka kuchakachua.

Naye Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini,David Kafulila alisema kuwa mkoa kigoma umekuwa mkoa wa vyama mbalimbali vya siasa vyenye wabunge kutoka vyama tofauti lakini Mama yake Zitto alikuwa mstari wa mbele katika kuwaunganisha kuwa wamoja kwa ajili ya maslahi ya mkoa Kigoma na watu wake.

na wabunge wa vingawa mkoa kigoma unaonyesha mkoa una mchanganyiko wa vyama mbalimbali vya siasa huyo mama aliwasaidia kuimarisha umoja wao.

Katika mazishi hayo CHADEMA iliwakislishwa na Mbunge wa jimbo la Nyamagana, Ezekie Wenje ambaye alisema kuwa shida Salum alikuwa kiongozi ambaye alisimamia kile anachokiamini wakati wa vikao vya kamati kuu na mikutano mbalimbali ya chadema.

Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Naibu waziri wa Fedha, Adam Malima, Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi, james Mbatia, mbunge wa Kigoma mjini, Peter serukamba, mbunge wa Kasulu mjini, Moses Machali, Mbunge wa Nkasi, ally Kesi, Mbunge wa tabora, Ismail Aden Rage, Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa.

Aidha pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa  mkoa kigoma ukiwakilishwa na Mkuu wa mkoa,Issa Machibya na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Walid Aman Kabourou ambapo Mkuu wa mkoa alisema kuwa amefarijika kuona mamia ya watu kutoka pande mbalimbali za nchi hii wakihudhuria mazishi ya mama shida jambo linaloonyesha kwamba alikuwa mtu aliyeishi na watu na kuwa msaada mkubwa kwao.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment