JESHI la kujenga taifa kikosi cha 821 Burombola mkoani
Kigoma imesema kuwa haitaweza kufikia malengo ya uzalishaji waliyowekewa na
makao makuu ya jeshi kutokana na kukabiliwa na mtaji mdogo na uharibifu wa
wadudu waharibifu.
Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili Mkuu wa
kambi hiyo, Meja Valentine Mrosso alisema kuwa kambi yake haitaweza kufikia
uzalishaji wa hekari 600 walizopewa kutokana na changamoto hizo.
Alisema kuwa tatizo la mtaji kifedha, uharibifu unaofanywa
na mchwa katika shamba la mahindi umechangia kurudisha nyuma malengo yao ya
uzalishaji na kwamba kwa mwaka huu kambi hiyo imeweza kulima hekari 350 pekee.
Aidha Meja Mrosso alisema kuwa kambi yake haipati pembejeo
za ruzuku ambazo zinatolewa kwa wakulima vijijini na serikali ambapo wameiomba
serikali kuwaingiza katika utaratibu wa kupata pembejeo za ruzuku jambo ambalo
litachangia kuwafanya waongeze uzalishaji.
Kwa upande wake meneja kilimo wa kambi hiyo, Adam Minzi
alisema kuwa pamoja na changamoto hizo zinazowakabili lakini wamejiwekea
malengo ya kuhakikisha wanalima hadi kufikia hekari 1000 katika kipindi cha
miaka miwili ijayo.
Minzi alisema kuwa tayari wameshatoa taarifa kwa idara ya
kilimo ya halmashauri ya wilaya kigoma kuhusiana na tatizo la mchwa ambao
wamekuwa wakishambulia mahindi yaliyoanza kukomaa na hivyo kurudisha nyuma
malengo ya uzalishaji.
Akizungumzia tatizo hilo Mkuu wa wilaya kigoma, Ramadhani
Maneno alisema kuwa pamoja na malengo yaliyowekwa ya kuongeza uzalishaji wa
mazao ya chakula katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo lakini pia kambi za JKT
na magereza mkoani humo ni maeneo ambayo mkoa unatarajia yatachangia kuongeza uzalishaji
katika utekelezaji wa mkakati wa kilimo kwanza.
Maneno alisema kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa idara ya
kilimo ya halmashauri ya wilaya kigoma kulifanyia kazi tatizo la mchwa
linaloikabili kambi hiyo ya Burombola ili kuweza kukabiliana na athari ambazo
zitaweza kutokea.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment