Saturday, February 9, 2013

BARAZA LA MADIWANI KUMC





Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji Alfred Luanda akizungumza katika baraza la madiwani la manispaa hiyo (kushoto) Meya wa manispaa Ujiji, Bakari Beji.


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 BARAZA la madiwani la Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji imeliomba jeshi la polisi nchini na mamlaka ya usalama wa usafiri wan chi kavu na majini (SUMATRA) waruhusu mabasi ya daladala katika manispaa hiyo kusimamisha abiria.

Wakizungumza wakati wa kikao cha kawaida cha baraza hilo baadhi ya madiwani ambao waliungwa mkono na Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Alfred Luanda wamesimamia hoja yao hiyo inakuja kutokana na ukweli kwamba kumekuwa na tatizo kubwa kwa askari wa usalama barabarani katika kushughulikia jambo hilo.

Akitoa hoja kuhusiana na hilo Diwani wa kata ya Katubuka, Moses Bilantanye alisema kuwa askari wa usalama barabarani wamekuwa wakiwakamata na kuwatoza faini wenye daladala kwa kusimamisha abiria ambapo alihoji kuwa kwa nini likatazwe kigoma na mikoa mingine iruhusiwe kusimamisha abiria.

Bilantanye alisema kuwa kitendo cha askari barabarani kuzuia daladala kutosimamisha abiria kunaleta taabu kwa wanafunzi na kuwafanya wachelewe shule lakini pia huwafanya watu wanaosafiri na magari hayo kutumia muda mrefu vituoni kutokana na kukatiliwa kupanda kwenye magari hayo kwa vile abiria wameenea kwenye viti.

Akiunga mkono jambo Hilo, Naibu Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Yunus Ruhonvya na mkurugenzi wake, Alfred Luanda wamezitaka mamlaka hizo kutengua sheria hiyo kwa manispaa ya Kigoma Ujiji kama ambavyo kwa kutumia busara zao wameweza kutengua sheria hiyo kwa jiji la Dar es salaam.

Akijibu kuhusiana na hilo,Mkuu wa usalama wa barabarani mkoa Kigoma,Michael Stephen alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya usalama barabara ya mwaka 1973 kifungu cha 39(a) ni marufuku kwa gari la abiria kubeba mzigo  kuzidi  uzito ulioandikishwa wakati gari hilo linayengenezwa.

Alisema kuwa hapa nchini kumekuwa na tabia ya wamiliki wa magari ya daladala kuzifanyia marekebisho gari zao kwa kuweka viti ambavyo vimefanya magari hayo kubeba abiria zaidi ya uzito ambao gari husika limeandikishwa lakini kwa busara mamlaka husika vimekuwa vikiacha jambo hilo likiendelea na kusimamia katika kuhakikisha abiria zaidi hawasimamishwi.

Hata hivyo alisema kuwa ni mchakato mrefu kuruhusu magari ya abiria kubeba abiria zaidi ya uzito wake kwani uzito ambao gari inapaswa kuchukua inazingatia suala la usalama wa gari na abiria waliokuwemo na kwamba ofisi yake haiwezi kuruhusu jambo hilo bila kuzingatia suala la uslama wa gari linapokuwa kwenye mwendo.

Naye afisa wa SUMATRA mkoa kigoma, Adam Mamilo alisema kuwa amelichukua ombi hilo na ataliwasilisha kwa viongozi wake ambao baada ya kulitafakari na kuwa na vikao na wadau mbalimbali ndipo jibu la nini kifanyike linaweza kutolewa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment