Friday, February 8, 2013



 Baadhi ya askari waliomaliza mafunzo ya kujitolea ya jeshi la kujenga taifa katika kambi ya JKT Burombola wilaya ya Kigoma wakiwa kwenye mazoezi ya kupita maeneo yenye vikwazo ili kumkaribia adui



Na Mwandishi wetu, Kigoma

JESHI la kujenga taifa kikosi cha 821 Burombola mkoani Kigoma imesema kuwa haitaweza kufikia malengo ya uzalishaji waliyowekewa na makao makuu ya jeshi kutokana na kukabiliwa na mtaji mdogo na uharibifu wa wadudu waharibifu.


Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili Mkuu wa kambi hiyo, Meja Valentine Mrosso alisema kuwa kambi yake haitaweza kufikia uzalishaji wa hekari 600 walizopewa kutokana na changamoto hizo.


Alisema kuwa tatizo la mtaji kifedha, uharibifu unaofanywa na mchwa katika shamba la mahindi umechangia kurudisha nyuma malengo yao ya uzalishaji na kwamba kwa mwaka huu kambi hiyo imeweza kulima hekari 350 pekee.


Aidha Meja Mrosso alisema kuwa kambi yake haipati pembejeo za ruzuku ambazo zinatolewa kwa wakulima vijijini na serikali ambapo wameiomba serikali kuwaingiza katika utaratibu wa kupata pembejeo za ruzuku jambo ambalo litachangia kuwafanya waongeze uzalishaji.


Kwa upande wake meneja kilimo wa kambi hiyo, Adam Minzi alisema kuwa pamoja na changamoto hizo zinazowakabili lakini wamejiwekea malengo ya kuhakikisha wanalima hadi kufikia hekari 1000 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.


Minzi alisema kuwa tayari wameshatoa taarifa kwa idara ya kilimo ya halmashauri ya wilaya kigoma kuhusiana na tatizo la mchwa ambao wamekuwa wakishambulia mahindi yaliyoanza kukomaa na hivyo kurudisha nyuma malengo ya uzalishaji.


Akizungumzia tatizo hilo Mkuu wa wilaya kigoma, Ramadhani Maneno alisema kuwa pamoja na malengo yaliyowekwa ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo lakini pia kambi za JKT na magereza mkoani humo ni maeneo ambayo mkoa unatarajia yatachangia kuongeza uzalishaji katika utekelezaji wa mkakati wa kilimo kwanza.


Maneno alisema kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa idara ya kilimo ya halmashauri ya wilaya kigoma kulifanyia kazi tatizo la mchwa linaloikabili kambi hiyo ya Burombola ili kuweza kukabiliana na athari ambazo zitaweza kutokea.


Mwisho.


No comments:

Post a Comment