Saturday, February 9, 2013

MIAKA 36 YA CCM - MATEMBEZI


Katibu wa siasa na uenezi wa CCM Taifa Nape Nnauye akiongoza akiwa mstari wa mbele katika matembezi ya mshikamano ya maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa CCM ambayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Jakaya kikwete Nyuma ya Nape ni Mkuu wa wilaya kigoma Ramadhani Maneno

Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Jakaya kikwete akifurahia ngoma iliyokuwa ikipigwa muda mfupi baada ya kumalizika kwa matembezi ya mshikamano ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma (Picha na Fadhili Abdallah)





MWENYEKITI wa CCM Taifa Jakaya Kikwete amesema kuwa chama hicho kimepania kuhakikisha kwamba mkoa Kigoma unapata maendeleo katika kipindi kifupi kijacho kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi badala ya kukalia maneno na kupiga majungu.

Akizungumza muda mfupi baada ya kumalizika kwa matembezi ya mshikamano ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa CCM alisema kuwa wakati huu ni wakati wa kuleta maendeleo mkoa kigoma.

Kikwete ambaye alichukua muda mchache kusalimia wananchi katika ofisi za CCM mkoa kigoma ambapo matembezi hayo ya mshikamano yaliishia alisema kuwa wamepania kwa dhati katika kusimamia jambo.

Alisema kuwa huu si wakati wa blabla na maneno ni wakati wao wanchi wa mkoa kigoma kupata maendeleo na kusisitiza kuwa jambo la muhimu wananchi na viongozi wa mkoa huo kuungana pamoja katika kuhakikisha mipango iliyowekwa ya maendeleo inatekelezwa bila vikwazo.

Awali Mwenyekiti wa CCM mkoa kigoma, Warid Aman Kabourou ameishukuru serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Raisi Jakaya Kikwete kwa kujali na kuonyesha kwa vitendo mkakati wa kuiletea kigoma maendeleo.

Kwa hali ya sasa Kabourou alisema kuwa haina haja ya kumwambia mtu aone kwani kila kitu kinajieleza chenyewe ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kuimarisha miundo mbinu, miradi ya kiuchumi na miradi ambayo ilikuwa kero kubwa kwa wananchi wa mkoa huo.

Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa CCM waandamizi wameeleza kuwa sherehe za miaka 36 ya CCM mkoani Kigoma imekuwa na mafanikio makubwa na hilo linatokana na namna ambavyo wananchi wa mkoa huo walivyoyapokea maadhimisho hayo.

Kotlida Kokupima kutoka wilaya ya Kasulu alisema kuwa majungu, fitina na migogoro baina ya viongozi wa chama hicho imechangia kupunguza mvuto wa chama kwa wananchi na kuchangia kwa viongozi wake kushindwa kuisimamia serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Aidha amepongeza serikali ya awamu ya nne kwa namna ambavyo imedhamiria kwa dhati na kwa vitendo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Kigoma jambo ambalo limerudisha imani ya wananchi kwa serikali na chama tawala.

Naye Rajabu Mwilima alisema kuwa uongozi wa sasa wa CCM unapaswa kusimamia maadili yake kikweli kweli hasa suala la vitendo vya rushwa katika chaguzi kwani vimekuwa vikishusha taswira nzuri ya chama hicho mbele ya jamii.

Mwilima alisema kuwa ana imani uongozi wa CCM ambao Makamu Mwenyekiti Philip Mangula ameingia utasaidia katika kurudisha taswira ya CCM kwenye kusimamia maadili ya uongozi, kanuni na uendeshaji wa chama ambao unajali maslahi ya jamii.

mwisho
 

No comments:

Post a Comment