Thursday, December 20, 2012

WAWILI WAUAWA KWA WIZI WA MBUZI


                                             Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WATU wawili wakazi wa kijiji Nyamtukuza wilaya ya kibondo mkoani Kigoma wameuawa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali wakituhumiwa kuiba mbuzi wawili wenye thamani ya shilingi 40,000.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraiser Kashai aliwataja watu hao waliouawa kuwa ni Nongo Bufinkri (36) na Azimio Muhabwa ambao waliiba mbuzi mali ya Sibalina John na waliuawa juzi majira ya mchana kijiji hapo.

Hata hivyo Kamanda Kashai alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambapo mtuhumiwa mmoja alifanikiwa kukimbia kabla ya wenzake kukutwa na mauti.

Katika tukio lingine kamanda huyo wa polisi mkoa kigoma alisema kuwa mkulima mmoja mkazi wa kijiji cha Kazuramimba Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma Stephano Muhunzi (70) aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni mjambazi.

Alisema kuwa katika tukio hilo watu watano walivamiwa nyumbani kwa marehemu majira ya mchana na baada ya kumjeruhi vibaya mwilini waliondoka na kondoo sita wenye thamani ya shilingi 300,000.

Aidha hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye amekamatwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo na kwamba juhudi za kuwatafuta wauaji zinaendelea.

Katika hatua nyingine Kamanda wa polisi mkoa kigoma, Fraiser Kashai amewataka wananchi mkoani Kigoma kujihadhari na watu wasiowema amabo wanafika kwenye makazi yao na kuwataka kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama wanapohisi kuna kitu cha namna hiyo.

Pia kamanda huyo wa polisi mkoa kigoma amesema kuwa jeshi lake limejipanga vizuri kuhakikisha kwamba kuna na amani na usalama wakati wote wa kipindi cha sikukuu za Christmas na mwaka mpya.

Mwisho.


RUN WAY AIRPORT KIGOMA

sehemu ya uwanja wa ndege Kigoma ambayo hivi sasa iko chini ya matengenezo kwa ajili ya kuifanya njia hiyo ya kurukia ndege kuwa ya kiwango cha lami

UKAGUZI UWANJA WA NDEGE KIGOMA

Waziri wa uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe katikati akitembelea na kukagua matengenezo ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami katika uwanja wa ndege wa Kigoma (wa kwa kulia) ni Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini, Dk.Agnes Kijazi.


Na Mwajabu Kigaza,Kigoma

WAZIRI wa uchukuzi Harison Mwakyembe ameitaka mamlaka ya viwanja vya ndege nchini kuhakikisha wananchi wa manispaa ya Kigoma ambao wanatakiwa kuhama kupishwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma wanalipwa katika kipindi kifupi kijacho.

Akizungumza muda mfupi baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa uwanja huo ambao unahusisha matengenezo ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami  Mwakyembe alisema kuwa hataki kusikia suala la fidia linakwamisha awamu ya pili ya upanuzi wa uwanja huo.

Akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa idara mbalimbali katika uwanja wa ndege wa Kigoma Waziri Mwakyembe alisema kuwa ni lazima hadi kufikia mwezi Februari mwaka ujao wakazi hao wawe wameshalipwa na mwezi Julai awamu ya pili ya uwanja huo iweze kuanza

Katika awamu ya kwanza ya mradi huo inahusisha ujenzi wa mita 1800 ya njia ya kurukia ndege kwa kiwango cha lami huku awamu ya pili ikihusisha kuendeleza urefu huo na kufikia mita 3100 ambazo zitawezesha ndege aina ya Boing 737 na air Bus kutua sambamba na ujenzi wa majengo mbalimbali uwanjani hapo ikiwemo jengo la kisasa la abiria.

Aidha pamoja na hatua nyingine Waziri huyo amesema kuwa ameridhishwa na kazi ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa kigoma inayofanywa na kampuni ya Syno Hydro ya China ambapo ameitaka kampuni kuhakikisha kwamba uwanja huo unafunguliwa katika kipindi kifupi kijacho ili kutoa nafuu ya usafiri wa ndege kwa wakazi wa mikoa ya Magharibi.

Alikusema kuwa kampuni hiyo imejenga imani  kubwa kwa serikali katika kuhakikisha inapewa  awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa uwanja huo kufikia hadhi ya uwanja wa ndege  wa kimataifa.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo mhandisi mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya stewart Scot International  ya Afrika Kusini , Cleopa Mpembeni amesema kuwa kumekuwa na maendeleo mazuri ya mradi huo katika awamu hii ya kwanza  na kwamba matarajio na kuhakikisha ujenzi huo unaisha kufikia mwezi Februari mwaka ujao.

Mpembeni alisema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili kwwa sasa ni kunyesha kwa mvua nyingi mkoani kigoma jambo ambalo limesababisha wakati mwingine kusimamisha kazi kwa siku  nzima au kufanya kazi hiyo nyakati za usiku.

Mwisho.

KUTUNUKU VYETI CHUO CHA HALI YA HEWA KIGOMA

Waziri wa uchukuzi Harison Mwakyembe (wa pili kushoto) akitunuku  cheti kwa amina Hussein (kulia) mmoja wa wahitimu 28 wa Diploma ya hali ya hewa wakati wa mahafali ya chuo cha hali ya hewa mjini Kigoma kwa mwaka huu 2012    (picha na Fadhili Abdallah)


Waziri wa uchukuzi Harison Mwakyembe  ameiagiza mamlaka ya hali ya hewa nchini( TMA) kufanya utafiti na kuon namna gani wanaweza kuwasaidia wananchi kukabiliana radi zinazotokea na kuwadhulu watu wengi nchini kila siku.


Akizungumza katika mahafali ya kuwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya diploma ya hali ya hewa katika chuo cha hali ya hewa kigoma Mwakyembe alisema kuwa n lazima wahitimu waonyeshe umahiri wao katika kuwasaidia wananchi kutokana na taaluma wanayopata.


Aalisema kuwa idara ya hali ya hewa imekuwa na umuhimu mkubwa kwa maisha ya wananchi lakini umuhimu huo usiishie kwenye utabiri tu lazima wasomi wanaohitimu mafunzo katika vyuo vya hali ya hewa ndani na nje ya nchi kuwasaidia wananchi kuona namna gani tenkolojia ya kukabiliana na radi inaweza kuwasaidia wananchi.


Aidha sambamba na hilo waziri huyo wa uchukuzi alisema kuwa mamlaka haina budi kurahisisha utabiri wa hali ya hewa na kuufanya uwe na manufaa ya moja kwa moja kwa mwananchi ili jamii na taifa liweze kupanga mipango yake kwa kuzingatia utabiri unaotolewa na idara hiyo.


Waziri Mwakyembe alisema kuwa ili kwenda na wakati na wananchi waone umuhimu wa uwepo wa taasisi hiyo  ni budi TMA  ianze kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa maeneo madogo pamoja na elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa.


kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini,Dk.A gnes kijazi amesema katika kuboresha shughuli za mamlaka , wako katika hatua za mwisho kwa kushirikiana na chuo kikuu cha Dar es salaam kuanza kutoa shahada ya hali ya hewa.


Dk.Kijazi alisema kuwa hata hivyo ufinyu wa bajeti umekuwa ukikwaza utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kimaendeleo ya mamlka hiyo na kwamba kwa mwaka ujao serikali imeahidi kuiongeza bajeti mamlaka hiyo ili iweze kutekeleza mipango yake kwa manufaa ya nchi.


kwa upande wao wahitimu wa mafunzo hayo , pamoja na kuelezea matumaini yao baada ya kumaliza masomo , wameiomba serikali kuyapatia ufumbuzi matatizo ya maabara, vitabu, majengo na usafiri yanayokikabili chuo hicho pekee cha hali ya hewa nchini.


Mmoja wa wahitimu hao, Shaban Dilunga  akisoma risala kwa niaba ya wajitimu hao alisema kuwa pamoja na changamoto hizo lakini ufinyu wa bajeti na uchache wa fedha wanazipowa umechangia kuwafanya washindwe kufanya mafunzo kwa vitendo (Field na study tour).


mwisho

KUHITIMU MAFUNZO YA MGAMBO




MKUU wa mkoa Kigoma Issa Machibya amewataka wahitimu wa kozi ya mgambo kuzingatia nidhamu na kutumia mafunzo hayo kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii badala ya kuwa chanzo cha kuwaingiza kwenye vitendo vya kihalifu.

Machibya alisema hayo katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma, Ramadhani Maneno wakati wa kufunga mafunzo ya mgambo kwa watumishi 168 wa serikali mkoani Kigoma yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa serikali ya mkoa imeamua kufanyika kwa mafunzo hayo lengo likiwa kuwajengea ukakamavu watumishi wake lakini pia kuongeza uzalendo miongoni mwa watumishi wake hasa vijan ambao wameanza kazi miaka ya hivi karibuni.

Awali katika risala ya wahitimu hao iliyosomwa kwa niaba yao na Noel Byamungu wamesema kuwa kumekuwa wamekuwambana na changamoto mbalimbali katika mafunzo hayo ikiwemo kitendo cha mwajiri kushindwa kuwalipa stahili zao kwa wakati.

Byamungu alisema kuwa kitendo kimechangia  kuwafanya washiriki kutoshiriki mafunzo kwa uhuru lakini kwani kimekuwa kikiharibu bajeti zao ambapo wameahidi kwamba watatumia mafunzo hayo kwa kadri ya kiapo walichokula kwa maslahi ya Watanzania wote.

Mwisho.

MSAADA WA BAISKELI KWA WATOA HUDUMA MAUMBANI

Mkuu wa wilaya Kasulu Dahn Makanga akimkabidhi baiskeli Thecla Mtereke mmoja wa watoa huduma kwa wagonjwa wa ukimwi majumbani na magonjwa sugu ili kuwawezesha watoa huduma hao kufanya kazi zao kwa urahisi anayeshuhhudia ni Sister Philipina Rubavu, Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki Kigoma



KANISA katoliki jimbo la kigoma limekabidhi baiskeli 88 zenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa watoa huduma kwa wagonjwa wa ukimwi majumbani wilayani Kasulu ili kuwawezesha kuzitumia baiskeli hizo kurahisisha mawasiliano kati yao na wagonjwa wanaowahudumia.

Baiskeli hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa wilaya kigoma, Dahn Makanga na Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki, Philipina Rubavu ambapo naye Mkuu wa wilaya Kasulu alikabidhi baiskeli hizo kwa watoa huduma 25 kwaniba ya watoa huduma wengine katika hafla iliyofanyika mjini Kasulu mwishoni mwa wiki iliyopita

Akikabidhi baiskeli hizo kwa watoa huduma Mkuu wa wilaya Kasulu, Dahn Makanga amewataka watoa huduma hao kuzitumia baiskeli hizo kuwafikia wagonjwa na kuwapatia msaada wanaohitaji.

Makanga alisema kuwa ni wazi kazi wanayofanya watoa huduma hao ni kubwa na hailingani na kiwango cha posho wanachopewa kwa kuwa wamekubali kujitoa na kwamba baiskeli hizo ziwe motisha kwao kupunguza adha kutembea umbali mrefu kuwafuata wagonjwa na kuwapatia huduma.

Naye Philipina Rubavu, Katibu Mtendaji wa idara ya afya jimbo Katoliki Kigoma alisema kuwa msaada huo umetolewa kupitia Tanzania Interfaith Partnership iliyo chini ya Tume ya Taifa ya kudhibiti ukimiw nchini (TACAIDS).

Alisema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali watoa huduma hao ambao pia wanajishughulisha na kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu wamekuwa na changamoto kubwa ya kufika maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa watoa huduma hao wanawahudhumia wagonjwa wa ukimwi wanaougulia majumbani na wagonjwa wengine zaidi ya 400 na watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi ya 1000 wakifanya kazi katika vijiji zaidi ya 25 wilayani humo.

Wakizungumzia msaada huo  baadhi ya watoa huduma hao walisema kuwa imekuwa faraja kubwa kwao kupata usafiri huo ambao utapunguza kwa kiasi changamoto ya usafiri wa kufikia maeneo mbalimbali ya utoaji huduma iliyokuwa ikiwakabili.

Thecla Mtereke na Laurian Ntamahurilo alisema kuwa kabla ya kupata baiskeli hizo walikuwa wakipata adha kubwa ya kutembea kwa mguu umbali mrefu kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa ajili ya kuwafuata wagonjwa wanaowahudhumia.

Mwisho.