Saturday, October 27, 2012

VIONGOZI WA DINI WATOA TAMKO KUHUSU VURUGU

a Fadhili Abdallah,Kigoma 

Viongozi wa madhehebu mbalimbali dini mkoani Kigoma wamekutana na kutoa tamko la pamoja la kulaani vitendo vilivyotokea vya kukojolea kitabu cha Quran, uchomaji makanisa na vurugu zinazoendelea nchini kwa kivuli cha imani ya kidini. 

Viongozi hao wa dini walisema hayo kwenye viwanja vya Mwanga Centre mjini kupitia baraza la mahusiano mema ya kidini katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya. 

Wa Kwanza kuzungumza katika mkutano huo alikuwa Katibu wa baraza kuu la waislam (BAKWATA) wilaya kigoma, Salum Kabunguru ambaye alisema kuwa baraza hilo linalaani kwa hali yeyote kitendo cha kukojolea kitabu kitukufu cha Quran kilichofanywa huko Mbagala Jijini Dar es Salaam.

 Sambamba na hilo kiongozi huyo wa BAKWATA alisema kuwa baraza hilo pia lina laani kwa nguvu zote uchomaji na uharibifu wa makanisa, kuharibifu makaburi kwa kuvunja misalaba na vurugu nyingine kwa imani ya misingi ya kidini ambayo inavunja amani na utulivu wa nchi. 

 Naye Mchungaji Charles Kitale,Mwenyekiti wa umoja wa makanisa mkoani Kigomaalisema kuwa uvumilifu na ustahimilivu miongoni mwa waumini wa madhehbu mbalimbali ya dini vinahitaji kupewa nafasi kwa kufuata maandiko ya vitabu vya dini zote. 

Alisema kuwa hakuna hata kitabu kimoja miongoni mwa vitabu vya dini ambavyo vinahimiza waumini wake kupigana na kuvuruga amani na utulivu vilivyokuwepo kwani hali hiyo haitoi nafasi kwa ibada za dini hizo kufanyika. .

 Akihitimisha matamko ya viongozi hao wa dini Katibu wa BAKWATA mkoa Kigoma, Moshi Guoguo ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la mahusiano mema ya kidini mkoani Kigoma alisema kuwa vurugu za aina yeyote kwa imani za misingi ya kidini hazikubaliki. 

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya ametaka viongozi wa dini na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini kuvumiliana na kuishi kwa upendo na kuonya kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuvuruga hali ya amani na utulivu iliyopo mkoani humo. 

Mwisho.

No comments:

Post a Comment