Na Fadhili
Abdallah,Kasulu
SERIKALI imesema
kuwa sekta ya afya nchini inakabiliwa na upungufu wa wataalam 62,000 sawa na
asilimia 49 ya wataalam wote wanaohitajika na kwamba serikali kupitia kwenye
vyuo vyake inatarajia kudahili wastani wa wanafunzi 10,000 kila mwaka kwa
kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Waziri Mkuu
Mizengo pinda amesema hayo katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Naibu
Waziri wa afya na ustawi wa jamii, Seif Rashidi wakati akifungua jengo la
upasuaji na jengo la wazazi la hospitali ya rufaa ya Misheni Kabanga iliyopo
wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Waziri mkuu
alisema kuwa ongezeko hilo kwa kiasi kikubwa limechangiwa na maboresho akubwa
yaliyofanywa kwenye sekta ya afya kwa kupanuliwa kwa hospitali za mikoa na
kuzifanya za rufaa na kupanuliwa kwa baadhi ya zahanati kufikia hadhi ya kuwa
vituo vya afya.
Alisema kuwa
pamoja na mkakati huo wa serikali bado kumekuwa na ongezeko kubwa la hospitali
na vituo vya afya vya watu binafsi na mashirika ya dini ambayo serikali
inapaswa kusaidia kwa namna yoyote.
Awali Mkurugenzi
wa hospitali ya Rufaa ya misheni Kabanga Sebastina Nzebayanga alisema kuwa
alisema kuwa hali ya umasikini inayowakabili wananchi wanoishi kuzunguka
hospitali hiyo imewafanya kutoza viwango vya chini vya malipo ya huduma
inayotolewa hali inayokwamisha kuajiri wataalam wenye sifa hospitalini hapo.
Alisema kuwa kwa
sasa hospitali hiyo haina daktari Bingwa wala daktari yeyote mwenye elimu ngazi
ya shahada na kwamba hiyo inatokana na kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za
mishahara na mahitaji mbalimbali ya wataalam.
Kwa upande wake
Meneja miradi wa tume ya kikristo ya huduma za jamii (CSSC), Grace Mwang’onda
alisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 900 zimetumika kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi hiyo zilizotolewa na serikali ya Ujerumani kupitia benki ya maendeleo
ya watu wa Ujerumani.
Mwang’onda alisema kuwa utekelezaji wa mradi
huo ni sehemu ya ushirikiano wa serikali za Tanzania na Ujerumani ambapo awamu
hii ya pili umehusisha ukarabati wa zahanati 44, uboreshaji wa hospitali nane
ikiwemo hiyo ya Kabanga ambayo imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment