Saturday, October 27, 2012

MASHEKHE WATAKA WAISLAM WASIUPAKE MATOPE UISLAM

Na Mwandishi wetu,Kigoma Ujiji 

WAUMINI wa dini ya kiislam mkoani Kigoma wameshiriki kwenye ibada ya Eid Alhaji kwa hali ya amani na utulivu ambapo viongozi wa dini na wale wa serikali wameihimiza waislam kudumisha amani na mshimamano miongoni mwa Watanzania. 

Wakizungumza katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo viongozi hao wamesema kuwa amani na usalama ndiyo msingi mkuu wa kuwezesha kufanyika kwa mambo mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa ibadi hiyo ya Eid El Haji. 

Akitoa mawaidha kwa waislama waliohudhuria ibada hiyo kwenye viwanja vya msikiti wa Kabondo Ujiji mjini Kigoma Kaimu Shekhe wa mkoa Kigoma, Hassan Iddi Kiburwa amesema kuwa imefika mahali waislama waondoe haya na kuwakemea wale wote wanaotaka kuvuruga amani kwa kisingizio cha dini. 

Akinukuu hadithi za mtume alisema kuwa Mtume aliamrisha watu wa umma wake kuwatendea wema na kuwasamehe wale wanaowakosea badala ya kulipiza kisasi na kuhimiza kuwa waislam kote nchini hawana budi kufuata mafundishi hayo kwani ndiyo msingi wa maisha ya kila siku ya Mwanadamu.

 Alisema kuwa hakuna mahali katika kurani ambako panamfundisha muumini wa dini ya kiislam kupigana au kufanya vitendo vinavyoashiria kuvuruga amani na usalama na kwamba vitendo hivyo vimekuwa vikiupaka matope uislam.

 Naye Mwenyekiti wa jumuia ya kuendeleza Kuran mkoani Kigoma, Hassan Kabeke alisema kuwa vitendo vya uvunifu wa amani na vurugu zinazoendelea nchini zimekuwa na maslahi ya kikundi fulani cha watu ambao wamekuwa wakiwachochea baadhi ya waislam kuungana mkono dhamira yao kwa kutumia dini. 

Alisema kuwa Waisla wanapaswa kulitambua hilo na kuwabaini watu hao ambao kwa namna yoyote hawataki kutii viongozi wao wala kutii mamlaka zilizopo ili kutumiza dhamira zao kwa faida zao binafsi na si kwa maslahi ya dini na waislam kwa ujumla wao. 

Akizungumza kwenye ibada ya Eid El Haji mjini hapa Mkuu wa wilaya kigoma Ramadhani Maneno alisema kuwa vitabu vya dini na hadithi ya mtume Muhamad zinahimiza waislam kupendana na kusameheana pale wanapokuwa wamekwaza na ameeleza kushangazwa na kitendo cha baadhi ya waislam kuhamasisha vurugu na uvunifu wa amani kwa kisingizio cha dini.

 mwisho

No comments:

Post a Comment