Saturday, October 27, 2012

KIKWETE AWAONYA WANAOVURUGA AMANI

Na Mwandishi Wetu,Kasulu

 Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa serikali haitawavumilia waumin wachache wa madhehebu ya dini wanaotaka kuvuruga amani ya nchi kwa maslahi yao na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kuhusika katika kuchochea vurugu za kidini zinazoendelea nchini. 

Raisi Kikwete alitoa kauli hiyo wilayani Kasulu mkoani Kigoma katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Bernad Membe wakati wa harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kanisa katoliki la mtakatifu petro mtume kigango cha Murubona wilayani kasulu.

 kwa upande wake kiongozi wa kanisa hilo , padre Castus Rwegoshora amesema kuwa zaidi ya shilingi milioni mia mbili zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo litakalokuwa na uwezo wa kuchukua waumin elfu mbili kwa wakati mmoja. 


 Katika harambee hiyo zaidi ya shilingi milioni sabini zilipatikana huku huyo wa mambo ya nchi za nje na rafiki zake wakichangia shilingi milioni hamsini.

 mwisho

WAUMINI WA DINI YA KIISLAM WAKIPEANA MKONO WA EID ELHAJI MKOANI KIGOMA

WAUMINI WA DINI YA KIISLAM WAKIPENA MKONO KUTAKIANA HERI NA FANAKA YA SIKUKUU YA EID ELHAJI BAADA YA KUMALIZIKA KWA SALA ILIYOFANYIKA KATIKA MSIKITI WA KABONDO UJIJI MKOANI KIGOMA ALIYESIMAMA KATI KATI NI KAIMU SHEIKH WA MKOA HASSA IDDI KIBURWA PICHA NA FADHILI ABDALLAH

Kigoma Press Club: SERIKALI YAELEZA UHABA MKUBWA WA WATAALAM WA AFYA

ASKOFU MKUU WA JIMBO LA TABORA AMBAYE PIA NI MSIMAMIZI WA JIMBO LA KIGOMA LA KANISA KATOLIKI PAUL RUZOKA AKIMUONGOZA NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII DK.SEIF RASHIDI (WA PILI KUSHOTO) NA MKUU WA MKOA KIGOMA ISSA MACHIBYA (WA KWANZA KUSHOTO) KUTEMBELEA MAJENGO YA HOSPITALI YA RUFAA YA KABANGA WILAYANI KASULU MKOANI KIGOMA (PICHA NA FADHILI ABDALLAH)






Na Fadhili Abdallah,Kasulu

SERIKALI imesema kuwa sekta ya afya nchini inakabiliwa na upungufu wa wataalam 62,000 sawa na asilimia 49 ya wataalam wote wanaohitajika na kwamba serikali kupitia kwenye vyuo vyake inatarajia kudahili wastani wa wanafunzi 10,000 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Waziri Mkuu Mizengo pinda amesema hayo katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa afya na ustawi wa jamii, Seif Rashidi wakati akifungua jengo la upasuaji na jengo la wazazi la hospitali ya rufaa ya Misheni Kabanga iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Waziri mkuu alisema kuwa ongezeko hilo kwa kiasi kikubwa limechangiwa na maboresho akubwa yaliyofanywa kwenye sekta ya afya kwa kupanuliwa kwa hospitali za mikoa na kuzifanya za rufaa na kupanuliwa kwa baadhi ya zahanati kufikia hadhi ya kuwa vituo vya afya.

Alisema kuwa pamoja na mkakati huo wa serikali bado kumekuwa na ongezeko kubwa la hospitali na vituo vya afya vya watu binafsi na mashirika ya dini ambayo serikali inapaswa kusaidia kwa namna yoyote.

Awali Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ya misheni Kabanga Sebastina Nzebayanga alisema kuwa alisema kuwa hali ya umasikini inayowakabili wananchi wanoishi kuzunguka hospitali hiyo imewafanya kutoza viwango vya chini vya malipo ya huduma inayotolewa hali inayokwamisha kuajiri wataalam wenye sifa hospitalini hapo.

Alisema kuwa kwa sasa hospitali hiyo haina daktari Bingwa wala daktari yeyote mwenye elimu ngazi ya shahada na kwamba hiyo inatokana na kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mishahara na mahitaji mbalimbali ya wataalam.

Kwa upande wake Meneja miradi wa tume ya kikristo ya huduma za jamii (CSSC), Grace Mwang’onda alisema kuwa kiasi cha shilingi milioni 900 zimetumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo zilizotolewa na serikali ya Ujerumani kupitia benki ya maendeleo ya watu wa Ujerumani.

 Mwang’onda alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya ushirikiano wa serikali za Tanzania na Ujerumani ambapo awamu hii ya pili umehusisha ukarabati wa zahanati 44, uboreshaji wa hospitali nane ikiwemo hiyo ya Kabanga ambayo imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa.

 Mwisho.
 

MASHEKHE WATAKA WAISLAM WASIUPAKE MATOPE UISLAM

Na Mwandishi wetu,Kigoma Ujiji 

WAUMINI wa dini ya kiislam mkoani Kigoma wameshiriki kwenye ibada ya Eid Alhaji kwa hali ya amani na utulivu ambapo viongozi wa dini na wale wa serikali wameihimiza waislam kudumisha amani na mshimamano miongoni mwa Watanzania. 

Wakizungumza katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo viongozi hao wamesema kuwa amani na usalama ndiyo msingi mkuu wa kuwezesha kufanyika kwa mambo mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa ibadi hiyo ya Eid El Haji. 

Akitoa mawaidha kwa waislama waliohudhuria ibada hiyo kwenye viwanja vya msikiti wa Kabondo Ujiji mjini Kigoma Kaimu Shekhe wa mkoa Kigoma, Hassan Iddi Kiburwa amesema kuwa imefika mahali waislama waondoe haya na kuwakemea wale wote wanaotaka kuvuruga amani kwa kisingizio cha dini. 

Akinukuu hadithi za mtume alisema kuwa Mtume aliamrisha watu wa umma wake kuwatendea wema na kuwasamehe wale wanaowakosea badala ya kulipiza kisasi na kuhimiza kuwa waislam kote nchini hawana budi kufuata mafundishi hayo kwani ndiyo msingi wa maisha ya kila siku ya Mwanadamu.

 Alisema kuwa hakuna mahali katika kurani ambako panamfundisha muumini wa dini ya kiislam kupigana au kufanya vitendo vinavyoashiria kuvuruga amani na usalama na kwamba vitendo hivyo vimekuwa vikiupaka matope uislam.

 Naye Mwenyekiti wa jumuia ya kuendeleza Kuran mkoani Kigoma, Hassan Kabeke alisema kuwa vitendo vya uvunifu wa amani na vurugu zinazoendelea nchini zimekuwa na maslahi ya kikundi fulani cha watu ambao wamekuwa wakiwachochea baadhi ya waislam kuungana mkono dhamira yao kwa kutumia dini. 

Alisema kuwa Waisla wanapaswa kulitambua hilo na kuwabaini watu hao ambao kwa namna yoyote hawataki kutii viongozi wao wala kutii mamlaka zilizopo ili kutumiza dhamira zao kwa faida zao binafsi na si kwa maslahi ya dini na waislam kwa ujumla wao. 

Akizungumza kwenye ibada ya Eid El Haji mjini hapa Mkuu wa wilaya kigoma Ramadhani Maneno alisema kuwa vitabu vya dini na hadithi ya mtume Muhamad zinahimiza waislam kupendana na kusameheana pale wanapokuwa wamekwaza na ameeleza kushangazwa na kitendo cha baadhi ya waislam kuhamasisha vurugu na uvunifu wa amani kwa kisingizio cha dini.

 mwisho

SHEKHE GUOGUO

MWENYEKITI WA KAMATI YA MAHUSIANO MEMA YA KIDINI MKOA KIGOMA AMBAYE PIA NI KATIBU WA BARAZA KUU LA WAISLAM (BAKWATA) MKOA KIGOMA SHEIKH SHABAN GUOGUO AKIZUNGUMZA WAKATI WA TAMKO LA VIONGOZI WA DINI KUHUSIANA NA VURUGU ZA KIDINI ZILIZOKUWA ZIKIENDELEA PICHA NA FADHILI ABDALLAH

VIONGOZI WA DINI WAKIIMBA WIMBO WA TAIFA

Viongozi wa madhehbu mbalimbali ya dini mkoani Kigoma wakiimba wimbo wa Tanzania Nakupenda wakati wa mkutano wa viongozi wa dini kutoa tamko kuhusiana na vurugu za kidini zinazoendelea nchini (wanne kushoto) ni Mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya.

VIONGOZI WA DINI WATOA TAMKO KUHUSU VURUGU

a Fadhili Abdallah,Kigoma 

Viongozi wa madhehebu mbalimbali dini mkoani Kigoma wamekutana na kutoa tamko la pamoja la kulaani vitendo vilivyotokea vya kukojolea kitabu cha Quran, uchomaji makanisa na vurugu zinazoendelea nchini kwa kivuli cha imani ya kidini. 

Viongozi hao wa dini walisema hayo kwenye viwanja vya Mwanga Centre mjini kupitia baraza la mahusiano mema ya kidini katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya. 

Wa Kwanza kuzungumza katika mkutano huo alikuwa Katibu wa baraza kuu la waislam (BAKWATA) wilaya kigoma, Salum Kabunguru ambaye alisema kuwa baraza hilo linalaani kwa hali yeyote kitendo cha kukojolea kitabu kitukufu cha Quran kilichofanywa huko Mbagala Jijini Dar es Salaam.

 Sambamba na hilo kiongozi huyo wa BAKWATA alisema kuwa baraza hilo pia lina laani kwa nguvu zote uchomaji na uharibifu wa makanisa, kuharibifu makaburi kwa kuvunja misalaba na vurugu nyingine kwa imani ya misingi ya kidini ambayo inavunja amani na utulivu wa nchi. 

 Naye Mchungaji Charles Kitale,Mwenyekiti wa umoja wa makanisa mkoani Kigomaalisema kuwa uvumilifu na ustahimilivu miongoni mwa waumini wa madhehbu mbalimbali ya dini vinahitaji kupewa nafasi kwa kufuata maandiko ya vitabu vya dini zote. 

Alisema kuwa hakuna hata kitabu kimoja miongoni mwa vitabu vya dini ambavyo vinahimiza waumini wake kupigana na kuvuruga amani na utulivu vilivyokuwepo kwani hali hiyo haitoi nafasi kwa ibada za dini hizo kufanyika. .

 Akihitimisha matamko ya viongozi hao wa dini Katibu wa BAKWATA mkoa Kigoma, Moshi Guoguo ambaye ni Mwenyekiti wa baraza la mahusiano mema ya kidini mkoani Kigoma alisema kuwa vurugu za aina yeyote kwa imani za misingi ya kidini hazikubaliki. 

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya ametaka viongozi wa dini na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini kuvumiliana na kuishi kwa upendo na kuonya kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kuvuruga hali ya amani na utulivu iliyopo mkoani humo. 

Mwisho.