Na Fadhili
Abdallah,Kigoma
USIMAMIZI wa
sheria za utunzaji na uhifadhi mazingira umekuwa ni changamoto kubwa katika
kuufanya mradi wa maendeleo ya bonde la ziwa Tanganyika kupata mafanikio kwani
kwa hali ya sasa mradi hauwezi kuchukua hatua kuhusiana na watu wanaoharibu
mazingira.
Meneja wa
Mradi huo, Hawa Mshamu alisema hayo katika ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo
ya utekelezaji wa mradi ziara inayotokana na mkutano wa siku moja wa wadau
kupeana taarifa ya hali ya maendeleo ya mradi huo.
Alikuwa
akijibu baadhi ya maswali ya wajumbe wa ziara hiyo waliotaka kujua uongozi wa
mradi unachukua hatua gani kwa watu wanaokaidi kutekeleza vipengele vya
utekelezaji wa mradi au wanaohareibu mazingira.
Mshamu
alisema kuwa kazi kubwa ya mradi ni kutoa elimu kwa jamii ya nini kifanyike kwa
manufaa ya siku za baadaye pamoja na kuendesha miradi mbalimbali ya utunzaji na
uhifadhi mazingira ikiwemo upandaji miti na miradi ya kujiingizia kipato kwa
jamii katika baadhi ya vijiji vya mradi huo.
Akizungumza katika
mkutano huo wa siku moja mkurugenzi wa mazingira wa mamlaka ya bonde la ziwa Tanganyika (LTA) Gabriel Hakizimana alisema kuwa yapo mafanikio ambayo
yameptaikana tangu kuanza kwa mradi ingawa zipo changamoto ambazo bado
zinatakiwa kufanyiwa kazi zaidi.
Hakizimana
alisema kuwa kikubwa zaidi elimu na uhamasishaji jamii unatakiwa kufanywa kwa
nguvu kubwa ili kuifanya jamii itambue umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa bonde
la ziwa Tanganyika kwa kipindi kirefu kijacho na kwamba vyombo vya habari
vinayo kazi kubwa katika kushiriki katika mkakati huo.
Mkurugenzi huyo
alisema kuwa ziwa Tanganyika ni urithi wa dunia likiwa na zaidi ya aina 600 za
viumbe ambapo kati yake 200 havipatikani mahali popote zaidi ya ndani ya ziwa
hilo na kwamba upo umuhimu mkubwa kwa
jamii inayozunguka ziwa hilo na nchi ambazo ziwa hilo lipo kulitunza kwa hali
na mali.
Akifungua
mkutano huo Mkuu wilaya kigoma, Ramadhani Maneno alisema kuwa wananchi
wanapaswa kulifanya suala la uhifadhi na utunzaji mazingira ya bonde la ziwa Tanganyika
kuwa sehemu ya maisha yao kutokana na umuhimu wa ziwa hilo.
Maneno
alisema kuwa pamoja na ufadhili wa wahisani wa nje lakini pia serikali itaweka
mkakati wa kuhakikisha fedha za utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika halmashauri
zinapatikana sambamba na kuzisimamia kwa karibu sheria za utunzaji na uhifadhi
huo wa mazingira.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment