Tuesday, June 12, 2012

JKT KANEMBWA MABINGWA WA SOKA KIGOMA


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

TIMU ya soka ya JKT Kanembwa ya wilaya ya kibondo mkoani Kigoma imefanikiwa kunyakua ushindi wa kwanza wa mashindano ya ligi ya taifa ngazi ya Taifa Kituo cha Kigoma baada ya kuibuka na pointi 16 ambazo hazikuweza kufikiwa na timu nyingine sita zilizoshiriki mashindano hayo.

katika mashindano hayo mabingwa hao waliweza kushinda michezo yao mitano na kutoka sare mchezo mmoja na hivyo ushindi huo unaipa tiketi timu hiyo ya Kigoma kucheza ligi daraja la kwanza nchini.

Ushindi wa pili katika kituo hicho cha Kigoma ulichukuliwa na timu ya mwadui ya shinyanga ambayo imeweza kufikisha point 11 baada ya kushinda michezo yake mitatu kutoa sare michezo miwili ambapo ilipoteza mchezo mmoja.


kufuatia kushika nafasi ya pili timu hiyo ya mwadui kutoka shinyanga italazimika kucheza ligi ndogo itakayojumuisha washindi wa pili kutoka vituo vingine ili kupata timu mbili zitakazoungana na timu zilizofuzu kwa ajili ya mshindano ya ligi daraja la kwanza.

Akizungumzia matokeo hayo Kocha wa timu ya JKT Kanembwa Saidi Mdoe amesema kuwa watalazimika kufanya usajili ili kupata wachezaji wa kukiongezea nguvu kikosi chake ili kifanye vizuri kuiwezesha timu hiyo kucheza ligi kuu nchini baada ya miaka 20 ya mkoa Kigoma kupotea katika mashindano hayo.


Kwa upande wake Katibu wa chama cha soka mkoa Kigoma Mrisho Bukuku amesema kuwa  timu hiyo inahitaji kupata wachezaji wenye uwezo wa kuhimili mikiki mikiki ya ligi hiyo daraja la kwanza na kuweza kuipandisha timu hiyo katika ligi kuu nchini.

katika kuunga mkono mafanikio ya timu hiyo Bukuku amesema kuwa uongozi wa serikali wilaya ya kibondo kwa kushirikiana na Mkuu wa mkoa Kigoma, Issa Machibya wamejipanga kutafuta fedha za kuiwezesha timu hiyo kufanya maandalizi ya kutosha na kupata mafanikio katika michezo yake.

mwisho

No comments:

Post a Comment