Sunday, June 30, 2013

WAKULIMA WA KAHAWA KIGOMA WAASWA KUTOKATA TAMAA




 Mwenyekiti wa chama kikuu cha wakulima wa tumbaku mkoa kigoma KANYOVU), Mathias Dangwa akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho (kulia) ni Meneja mkuu wa KNYOVU, Jeremia Nkangaza.



Na Mwandishi Wetu, Kigoma

CHAMA  kikuu cha wakulima wa kahawa mkoa kigoma (KANYOVU)  kimewataka wakulima wa mkoa huo kutokata tamaa na kuanguka kwa bei katika soko la dunia badala yake kuhakikisha kwamba kahawa inayozalishwa inakuwa na ubora wa juu jambo ambalo ndiyo njia pekee ya kuwafanya kuwa na soko la uhakika.

Akizungumza katika mkutano Mkuu wa chama hicho kinachojumuisha vyama vya msingi 11 vya wakulima wa kahawa mkoani Kigoma Meneja wa Kanyovu Jeremia Nkangaza amesema kuwa kupanda na kushuka kwa bei kwenye soko la dunia ni jambo la kawaida na kwamba wakulima wategemee kitu kama hicho kutokea.

Wasi wasi wa kushuka bei kwa kahawa katika soko la dunia kunafuatia mkakati wa nchi ya Brazili ambayo ni mzalishaji mkubwa wa kahawa duniani kuongeza uzalishaji hali ambayo itaathiri bei katika nchi changa zinazozalisha kahawa.

Alisema kuwa katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya bei katika soko la dunia mkakati wa chama hicho ni kuhakikisha wanazalisha kwa ubora wa juu na kupata masoko ya moja kwa moja badala ya kuendelea kupambana katika minada.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanyovu, Mathias Dangwa amesema kuwa pamoja na changamoto ya masoko katika soko la dunia lakini pia amelalamikia kutokuwepo kwa wataalam wa kahawa kwa ajili ya kutoa maelekezo kwa wakulima katika kusimamia uzalishaji unaozingatia ubora.

Sambamba na suala la wataalam Dangwa amesema kuwa upatikanaji wa pembejeo na madawa nalo ni tatizo na hakuna maelekzo ya moja kwa moja ya kitaalam ya aina ya madawa ya kutumia na hali hiyo inafanya kila mmoja kutumia madawa ambayo anadhani anayamudu kulingana na bei.

Kaimu Afisa kilimo wa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Siwajibu Selemani amekiri kuwepo kwa wataalam wachache wa kahawa katika halmashauri hiyo lakini mkakati wa serikali ni kuhakikisha wataalam wanapatikana na kuwafikia wakulima kwa wakati.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment