Sunday, June 30, 2013

KANISA LA TAG KIGOMA LAWEKWA WAKFU

Askofu Mkuu wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo la Kanisa la TAG Jimbo la Kigoma  

 Waumini wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiwa wameshika kuta za jengo la kanisa hilo ikiwa ishara ya kuliombea na kuliweka WAKFU.





MAASKOFU, wachungaji na viongozi mbalimbali wa makanisa mkoani Kigoma wakiwa wameshika kuta za kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiliombea na kuliwekea WAKFU kama ishara ya kulizindua rasmi jengo hilo.
 
 
Na Mwandishi wetu, Kigoma
 
ASKAFU Mkuu wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali amepiga marufuku viongozi na waumini wa kanisa hilo kutumia nyumba za ibada za kanisa hilo kuendeshea masuala ya kisiasa.
 
Mtokambali alisema hayo alipokuwa akitoa hotuba  wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la kanisa la TAG jimbo la Kigoma ambapo askofu huyo alisema kuwa kama kiongozi mkuu wa TAG hatasita kumfukuza kiongozi au muumini yeyote ambaye atabainika kutumia majengo ya kanisa kuendesha shughuli za kisiasa.
 
Alisema kuwa kuingiza masuala ya kisiasa katika nyumba za ibada kumekuwa na athari kubwa katika uendeshaji wa kanisa na kwamba matukio yanayotokea maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kulipuliwa kwa mabomu kwa waumini kanisani msingi wake  ni kuacha kuabudu na badala kuendesha siasa.
 
Aliwaasa vipongozi na wamumini wa kanisa hilo kwamba nyumba za ibada zinapaswa kuheshimiwa kama mahali pa takatifu na kudumishwa kama sehemu takatifu ambapo wenye kukata tama watakimbilia kuokolewa.
 
Mtokambali alisema kuwa katika siku za karibuni kumekuwa na matendo mbalimbali ya kisiasa na uvunjifu wa amani ambapo waumini wa nyumba za ibada wanaendeha maandamano na kubeba mabango katika kuwakataa viongozi wa madhehebu yao badala ya kutumia vikao vya kikatiba vya makanisa yao.
 
Alisema kuwa TAG imekuwa ikiwafukuza viongozi na waumini wake kutoka katika kanisa hilo kwa utovu wa nidhamu na kwenda kinyume na maadili ya kanisa kwa sababu suala hilo lilianza tangu kwa Mungu ambapo shetani alifukuzwa na Mungu baada ya kuasi.
 
Sambamba na hilo Askofu huyo ameonya kuwepo kwa vitendo vya ubaguzi, ukabila na unyanyapaa miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na kwamba vitendo hivyo pia havitavumiliwa ndani ya kanisa na kuwataka maaskofu na wachungaji kusimamia wajibu wao katika kusimamia kanisa.
 
Awali akisoma risala kwa niaba ya Kanisa hilo mzee wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Alembe Sadock amesema kuwa jumla ya shilingi milioni 94.7 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo kutoka katika mkakati wa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 95.3 na kwamba ili liweze kukamilika kabisa kiasi cha shilingi milioni 55 nyingine zinahitajika kuweza kumalizia ujenzi huo.
 
Alisema kuwa sababu ya kanisa kushindwa kukamilika kama ilivyokusudiwa awali ni pamoja na kupanda kwa gharama za vifaa na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa vifaa vya ujenzi kutoka maeneo ya nje ya mkoa Dar es salaam.
 
Kwa upande wake Mchungaji Kiongozi wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Omari Mlenda amesema kuwa hadi sasa kanisa hapo lilipofikia hakuna msaada wowote kutoka nje ya nchi ambao umetumika na kwamba sehemu kubwa ya fedha za ujenzi wa kanisa hilo zimetoka kwa wauimini wenyewe.
 
Kwa sasa mchungaji Mlenda amesema kuwa wauimini na wadau mbalimbali wa kanisa hilo wanahitaji kujitoa tena kuweza kupata kiasi cha shilingi milioni 55 ambazo zitatumika kumaliza sehemu ya paa ya kanisa hilo na maeneo machache yaliyobaki.
 
Mwisho.
 

No comments:

Post a Comment