Askofu Mkuu wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo la Kanisa la TAG Jimbo la Kigoma
Waumini wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiwa wameshika kuta za jengo la kanisa hilo ikiwa ishara ya kuliombea na kuliweka WAKFU.
MAASKOFU, wachungaji na viongozi mbalimbali wa makanisa mkoani Kigoma wakiwa wameshika kuta za kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiliombea na kuliwekea WAKFU kama ishara ya kulizindua rasmi jengo hilo.
Na Mwandishi wetu, Kigoma
ASKAFU Mkuu
wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali amepiga
marufuku viongozi na waumini wa kanisa hilo kutumia nyumba za ibada za kanisa
hilo kuendeshea masuala ya kisiasa.
Mtokambali alisema
hayo alipokuwa akitoa hotuba wakati wa
ufunguzi wa jengo jipya la kanisa la TAG jimbo la Kigoma ambapo askofu huyo
alisema kuwa kama kiongozi mkuu wa TAG hatasita kumfukuza kiongozi au muumini
yeyote ambaye atabainika kutumia majengo ya kanisa kuendesha shughuli za
kisiasa.
Alisema kuwa
kuingiza masuala ya kisiasa katika nyumba za ibada kumekuwa na athari kubwa
katika uendeshaji wa kanisa na kwamba matukio yanayotokea maeneo mbalimbali
nchini ikiwemo kulipuliwa kwa mabomu kwa waumini kanisani msingi wake ni kuacha kuabudu na badala kuendesha siasa.
Aliwaasa
vipongozi na wamumini wa kanisa hilo kwamba nyumba za ibada zinapaswa
kuheshimiwa kama mahali pa takatifu na kudumishwa kama sehemu takatifu ambapo
wenye kukata tama watakimbilia kuokolewa.
Mtokambali
alisema kuwa katika siku za karibuni kumekuwa na matendo mbalimbali ya kisiasa
na uvunjifu wa amani ambapo waumini wa nyumba za ibada wanaendeha maandamano na
kubeba mabango katika kuwakataa viongozi wa madhehebu yao badala ya kutumia vikao
vya kikatiba vya makanisa yao.
Alisema kuwa
TAG imekuwa ikiwafukuza viongozi na waumini wake kutoka katika kanisa hilo kwa
utovu wa nidhamu na kwenda kinyume na maadili ya kanisa kwa sababu suala hilo
lilianza tangu kwa Mungu ambapo shetani alifukuzwa na Mungu baada ya kuasi.
Sambamba na
hilo Askofu huyo ameonya kuwepo kwa vitendo vya ubaguzi, ukabila na unyanyapaa
miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na kwamba vitendo hivyo pia havitavumiliwa
ndani ya kanisa na kuwataka maaskofu na wachungaji kusimamia wajibu wao katika
kusimamia kanisa.
Awali akisoma
risala kwa niaba ya Kanisa hilo mzee wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Alembe
Sadock amesema kuwa jumla ya shilingi milioni 94.7 zimetumika kwa ajili ya
ujenzi wa kanisa hilo kutoka katika mkakati wa kukusanya kiasi cha shilingi
milioni 95.3 na kwamba ili liweze kukamilika kabisa kiasi cha shilingi milioni
55 nyingine zinahitajika kuweza kumalizia ujenzi huo.
Alisema kuwa
sababu ya kanisa kushindwa kukamilika kama ilivyokusudiwa awali ni pamoja na
kupanda kwa gharama za vifaa na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa vifaa
vya ujenzi kutoka maeneo ya nje ya mkoa Dar es salaam.
Kwa upande
wake Mchungaji Kiongozi wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Omari Mlenda amesema
kuwa hadi sasa kanisa hapo lilipofikia hakuna msaada wowote kutoka nje ya nchi
ambao umetumika na kwamba sehemu kubwa ya fedha za ujenzi wa kanisa hilo
zimetoka kwa wauimini wenyewe.
Kwa sasa
mchungaji Mlenda amesema kuwa wauimini na wadau mbalimbali wa kanisa hilo
wanahitaji kujitoa tena kuweza kupata kiasi cha shilingi milioni 55 ambazo
zitatumika kumaliza sehemu ya paa ya kanisa hilo na maeneo machache yaliyobaki.
Mwisho.