Na Fadhili
Abdallah,Kigoma
Wadau wa habari mkoani Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni Rasmi Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser Kashai siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma
Waandishi wa habari kutoka chama cha waandishi wa habari mkoani Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser kashai mwenye kofia waliokaa wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma (Picha zote na Fadhili Abdallah)
Na Mwandishi wetu, Kigoma
WAANDISHI wa
habari mkoani Kigoma wametakiwa kutumia kalamu zao kwa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari kwani zikitumika vizuri zinaweza kuwa
chachu na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya jamii na kwamba kinyume
chake kalamu za waandishi zinaweza kugeuka risasi na kuleta maafa makubwa kwa
jamii.
Diwani wa kata ya
Mwanga Kaskazini, Francis Mangapi alisema hayo katika kilele cha maadhimisho ya
siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma yaliyoratibiwa na chama cha
waandishi wa habari mkoani humo (KGPC).
Mangapi alisema
kuwa tumeshuhudia maeneo mbalimbali ambapo waandishi wametumika vizuri kumekuwa
na maendeleo makubwa na jamii imehamasika katika kujieleta maendeleo lakini
mahala ambapo waandishi wametumika vibaya kumekuwa na matatizo makubwa makubwa.
Akichangia
kuhusiana na jambo hilo Mfanyabiashara maaruru wa mjini Kigoma Miforo
Mpozemenya alisema kuwa waandishi wa habari wasikubali kutumiwa na wanasiasa
ama makundi mbalimbali kwa faida zao badala yake wajikite katika kufanya
kazi kwa kuzingatia maslahi ya jamii na kufuata maadili ya taaluma yao.
Akizungumza
katika maadhimisho hayo Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Fraisser Kashai ambaye
alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo baina
ya waandishi na jeshi lake lakini waandishi wa habari wamekuwa mchango mkubwa
katika kufanikisha mambo mbalimbali ya kiutendaji ndani ya jeshi la polisi.
Kashai alisema
kuwa jeshi lake litaendelea kutoa msaada na kushirikiana na vyombo vya habari
kwa kadri iwezekanavyo na kwamba kama kuna kutoelewana mahali baina yao ofisi
yake iko wazi muda wote kwa ajili ya majadiliano na kuzungumza namna gani ya
kuweza kufanya kazi pamoja.
Awali Mwenyekiti
wa chama cha waandishi wa habari mkoa kigoma, Deogratius Nsokolo, matukio ya
hivi karibuni ya kuuawa kwa mwandishi wa habari,Daudi Mwangosi wa Iringa, Issa
Ngumba wa Kibondo mkoani Kigoma na kuteswa na kutobolewa jicho kwa Mwenyekiti
wa jukwaa la wahariri Tanzania, Absolom Kibanda kunawafanya waandishi wa habari
watafakari namna ya utekelezaji wa majukumu yao.
Hata hivyo
Nsokolo alisema kuwa matukio hayo badala ya kuwarudisha nyuma na kuwavunja moyo
badala yake vimewapa ari , ujasiri na mbinu mpya waandishi wa habari
katika kuendeleza majukumu yao lakini pia kufichua mambo
mabaya ambayo yanafanywa na watu wachache huku mambo hayo ikiacha jamii kubwa
ya Watanzania ikiteseka.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment