Sunday, May 19, 2013

KIKAO CHA MAHAKAMA KUU KIGOMA

 Jaji wa mahakama kuu kanda ya Tabora Sam Mpaya Rumanyika akikagua gwaride la askari wa kikosi cha kutulia ghasia ikiwa ishara ya kuanza kwa kikao cha mahakama kuu mkoani Kigoma


Jaji wa mahakama kuu kanda ya Tabora Sam Mpaya Rumanyika akipokea salamu za utii kutoka kwa kikosi cha askari wakutuliza ghasia (Hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kikao cha mahakama kuu kanda ya Tabora mkoani Kigoma (kulia) ni Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser Kashai na nyuma ni watumishi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa mkoa kigoma Issa machibya

WADAU WA HABARI KIGOMA

 Wadau wa habari mkoani Kigoma wakifuiatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolwa siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma.


Kamanda wa polisi Fraisser Kashai ambaye alikuwa mgeni rasmi siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma akitoa hotuba yake kwa washiriki wa maadhimisho hayo

SIKU YA UHURU WA HABARI NCHINI

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Kigoma Deo Nsokolo (kushoto) akizungumza katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani aliyekaa kati kati Ni Kamanda wa polisi mkoa kigoma Fraisser Kashai aliyekuwa mgeni rasmi na kulia Afisa habari ofisi ya mkuu wa mkoa kigoma, Edward Ng'onoli


Wadau wa habari mkoani Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni Rasmi Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser Kashai siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma
 
Waandishi wa habari kutoka chama cha waandishi wa habari mkoani Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser kashai mwenye kofia waliokaa wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma (Picha zote na Fadhili Abdallah)

 
Na Mwandishi wetu, Kigoma
 
WAANDISHI wa habari mkoani Kigoma wametakiwa kutumia  kalamu zao kwa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari kwani zikitumika vizuri zinaweza kuwa chachu na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya jamii na kwamba kinyume chake kalamu za waandishi zinaweza kugeuka risasi na kuleta maafa makubwa kwa jamii.

Diwani wa kata ya Mwanga Kaskazini, Francis Mangapi alisema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma yaliyoratibiwa na chama cha waandishi wa habari mkoani humo (KGPC).

Mangapi alisema kuwa tumeshuhudia maeneo mbalimbali ambapo waandishi wametumika vizuri kumekuwa na maendeleo makubwa na jamii imehamasika katika kujieleta maendeleo lakini mahala ambapo waandishi wametumika vibaya kumekuwa na matatizo makubwa makubwa.

Akichangia kuhusiana na jambo hilo Mfanyabiashara maaruru wa mjini Kigoma Miforo Mpozemenya alisema kuwa waandishi wa habari wasikubali kutumiwa na wanasiasa ama makundi mbalimbali kwa faida zao badala  yake wajikite katika kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya jamii na kufuata maadili ya taaluma yao.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Fraisser Kashai ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo baina ya waandishi na jeshi lake lakini waandishi wa habari wamekuwa mchango mkubwa katika kufanikisha mambo mbalimbali ya kiutendaji ndani ya jeshi la polisi.

Kashai alisema kuwa jeshi lake litaendelea kutoa msaada na kushirikiana na vyombo vya habari kwa kadri iwezekanavyo na kwamba kama kuna kutoelewana mahali baina yao ofisi yake iko wazi muda wote kwa ajili ya majadiliano na kuzungumza namna gani ya kuweza kufanya kazi pamoja.

Awali Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa kigoma, Deogratius Nsokolo, matukio ya hivi karibuni ya kuuawa kwa mwandishi wa habari,Daudi Mwangosi wa Iringa, Issa Ngumba wa Kibondo mkoani Kigoma na kuteswa na kutobolewa jicho kwa Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania, Absolom Kibanda kunawafanya waandishi wa habari watafakari namna ya utekelezaji wa majukumu yao.

Hata hivyo Nsokolo alisema kuwa matukio hayo badala ya kuwarudisha nyuma na kuwavunja moyo badala yake vimewapa ari , ujasiri na mbinu mpya waandishi wa habari    katika kuendeleza majukumu yao lakini pia kufichua mambo mabaya ambayo yanafanywa na watu wachache huku mambo hayo ikiacha jamii kubwa ya Watanzania ikiteseka.

Mwisho.

WANAOHAMISHWA KIBIRIZI WALALAMIKIA FIDIA KUCHELEWA


Na Fadhili Abdallah,Kigoma


wafanyabiashara na wananchi waliokuwa wakiishi na kufanya shughuli zao katika eneo la bandari ndogo ya kibirizi Manispaa ya kigoma ujiji, wamelalamikia hatua ya manispaa hiyo kuchelewesha kuwalipa malipo yao ya fidia na kuwazuia kufanya shughuli zozote za kujiingizia kipato.


Wakizungumza katika mahojiano maalum na gazeti  wananchi hao wamesema kuwa baada ya kufanywa tathmini ya upanuzi wa bandari ndogo ya Kibirizi manispaa ya Kigopma Ujiji zaidi ya mwaka mmoja uliopita   lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.


Mmoja wa wananchi hao Patrick Ntahondi alisema kuwa amekuwa na hali ngumu kimaisha kwani hawezi kufanya lolote katika eneo lake kwa sasa kwa sababu watu wengi wameshahama na kuhamisha shughuli zao lakini wao hawaelewi mambo yakoje na kuwawia ngumu kuendesha maisha yao.


Naye Jasmine Katekwe alisema kuwa ana nyumba yake katika eneo hilo ambayo alikuwa akiitumia kupangisha wafanyabishara kuhifadhi mizigo yao na pia kuwapa eneo la kukaushia samaki na dagaa lakini serikali imesimamisha shughuli za biashara na hali kiuchumi kwake imekuwa ngumu.


Sambamba na hilo alisema kuwa anashindwa kufanya marekebisho yeyote katiuka nyumba yake kutokana na serikali kueleza kwamba tayari tathmini imeshafanyika ambapo wameiomba serikali kuingilia kati na kuwaruhusu waendelee na shughuli za kuwaingizia kipato na makazi.



Akizungumzia jambo hilo Naibu Meya wa Manispaa ya Kigoma Rashidi Ruhonvya  amesema kuwa kuchelewa kulipwa fidia kwa wananchi wa eneo hilo kumetokana na kukosewa kwa tathmini ya awali baada ya kuwepo kwa baadhi ya wananchi ambao hawakujumuishwa licha ya maeneo na vibanda vyao kubainishwa.

Alisema kuwa tayari muhakiki ameshafika na anaipitia upya repoti ya tathmini kuona kama kuna itilafu mahali na kwamba baada ya kufanyiwa marekebisho kwa itililafu zilizojitokeza malipo ya watu hao yatafanywa haraka iwezekanavyo na kwani uhakiki huo umefikia hatua ya mwisho.


Hata hivyo Ruhovya ametoa wito kwa watu wote waliokuwa wakiishi na kufanya shughuli mbalimbali katika eneo hilo kusitisha mambo hayo wasubiri kulipwa fidia zao na kutafuta maeneo mengine kwa ajili ya makazi na shughuli zao.

Mwisho.


ILI kuhakikisha wanawatumia watoto wao katika shughuli zao za kiuchumi badala ya kuwa shuleni imebainika kuwa wazazi wengi katika vijiji mbalimbali vya  wilayani Kibondo  wanakaidi kwa makusudi kuwalipia ada na michango mbalimbali watoto waliofaulu na kuchaguliwa  kujiunga na masomo ya sekondari wilayani humo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti na kuthibitishwa na ngazi mbalimbali za uongozi wa kiserikali na kijamii imethibitisha kwamba  vitendo hivyo vimefanya uongozi wa shule za sekondari katika wilaya hiyo na serikali za vijiji na kata kutumia muda mrefu katika kuhangaika kuwaokoa watoto hao na vitendo vya wazazi wao.

Akithibitisha kuhusiana na hilo Mkuu wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kumgogo tarafa ya Mabamba wilayani humo, Adolf Tuseko alisema kuwa vitendo vya wazazi kukaidi kuwalipia ada watoto kwa makusudi vimechukua nafasi kubwa ya shughuli za utawala shuleni hapo zaidi ya shughuli za kitaaluma.

Mkuu huyo wa shule alithibitisha kwamba wazazi wanatumia hila ya kutokuwa na fedha za kuwalipia watoto wao ili watoto hao watakaporudishwa nyumbani iwe rahisi kwao kuwatumia kwa shughuli za kufanya vibarua kwenye mashamba na biashara kwenye magulioa.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo wanalazimika kulipeleka suala hilo katika uongozi wa kata ambapo majina ya wazazi ambao wanachukua muda mrefu kutolipa michango hiyo hupelekwa huko na mtendaji wa kata na baraza la maendeleo la kata ndiyo husimamia hilo.

Akizungumzia kuhusiana na hilo Mwalim Mkuu wa shule ya Msingi Mkarazi, Asumwisye Peter alisema kuwa  pamoja na madai ya kipato kidogo cha wazazi lakini wazazi wengi hawana mwamko wa elimu na ndiyo maana hawaoni umuhimu wa watoto wao kuendelea na masomo ya sekondari.

Alisema kuwa kabla ya ujenzi wa sekondari za kata watoto wengi walikuwa wakiishia darasa la saba na wazazi walikuwa wakipata nafasi ya kuwatumia watakavyo na kuwafanya ndiyo chanzo cha kuingiza mapato kwa ajili ya kuendesha familia kutokana na kutumika kwenye kufanya kazi za vibarua.

Anasema kuwa wakati mwingine hasa wakati wa magulio au wakati wa kilimo watoto wengi hutolewa shuleni na kwenda kufanya kazi kwenye mashamba au masoko na hiyo si kwa shule za msingi tu bali hata kwa shule za sekondari na imekuwa ni tatizo kubwa kati ya shule na jamii inayozunguka shule hizo ambao watoto wao wanasoma hapo.

Kwa upande wake mmoja wa wazazi walioongea na gazeti hili, Method Kalumanzila alithibitisha kwamba kitendo cha wazazi kutolipa ada na pia kuwatoa watoto shule kwa ajili ya kwenda kufanya vibarua imekuwa tatizo sugu na kikubwa ni mwamko mdogo wa wazazi katika elimu na hali duni ya kipato kwa wazazi.

Naye Mzazi mwingine, Magreth Sunzu mfanyabiashara katika soko la Mabamba alisema kuwa  wazazi hawaoni umuhimu wa watoto wao kuendelea na masomo ya sekondari kwa sababu baada ya miaka minne ya masomo wengi huambilia alama sifuri (Division Zero) na kubaki nyumbani kama wenzao walioishia darasa la saba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Leopold  Ulaya alithibitisha matatizo hayo mawili kuikabili wilaya yake na kusema kuwa wamo katika mchakato wakuona wafanye nini kukabiliana na hali hiyo lakini kwa sasa uongozi wa kata umepewa mamlaka ya kuwachukulia hatua wazazi kwa kuwafikisha kwenye baraza la kata na kuwatoza faini.

Sambamba na hilo alisema kuwa wanatarajia kutembelea halmashauri ambazo zinachamoto kama ya kwao ili kuona namna gani wanafanya kukabiliana na hali hiyo lakini pia wanawaza namna ya kutunga sheria ndogo za halmashauri ambazo zitawabana na kuhakikisha kwamba wanalipa michango ya watoto wao na pia kuhakikisha kwamba watoto wao kuhudhuria masomo.

Mkuu wa wilaya kibondo kwa upande wake alisema kuwa utoro kwa wanafunzi wa sekondari kuacha masomo na kwenda kufanya shughuli za biashara na vibarua ni tatizo kubwa lakini pia suala la wazazi kukataa kulipia gharama za masomo ya watoto wao ni tatizo lingine ambayo kwa pamoja wanayatarajia kuyafanyia kazi katika kikao cha wadau wa elimu wanachotarajia kuitisha.

Mwisho.