UVINZA FM SASA HEWANI
Mwandishi wa habari Mwandamizi Fadhili Abdallah akiwa katika studio za Uvinza FM ambayo inarusha matangazo yake kutoka kwenye mji mdogo wa Uvinza mkoani Kigoma.
Wakazi wa wilaya ya UVINZA na
vijiji vya jirani mkoani KIGOMA wamenufaika na uzinduzi wa mradi wa
UVINZA FM utakaotumika kuhamasisha, amani, demokrasia na maendeleo .
Mradi
huo umezinduliwa hivi karibuni katika ukumbi wa vijana UVINZA ukiwa ni
miongoni mwa Redio 26 zinazotekeleza barani afrika ikiwa ni mchakato wa
demokrasia kupitia vyombo vya habari.
Mradi huo unaofadhiliwa
na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na
Utamaduni- UNESCO kwa kushirikiana na Shirika jingine la Umoja wa
Mataifa la Mpango wa Maendeleo -UNDP.
Katika hotuba iliyosomwa
na mkuu wa wilaya ya UVINZA Bi. HADIJA NYEMBO kwa niaba ya mkuu wa mkoa
LUTENI KANALI MSTAAFU ISSA MACHIBYA amehimiza utendaji kazi kwa bidii na
utekelezaji wa majukumu ya UVINZA FM ili kukuza na kudumisha
mawasiliano yatakayosaidia wananchi kufikisha matatizo na kero zao kwa
urahisi .
Ameahidi kutoa ushirikiano kwa kupitia wananchi
kuhakikisha mradi huo unafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Ameishukuru Aitel
Tanzania kwa mchango wake wa kuruhusu mitambo ya Radio UVINZA F.M
kufungwa katika minara hiyo.
Akizungumza Mkurugenzi wa UVINZA
F.M bwana AYOUB KALUFYA amewaasa wanawake watumie fursa ya radio hiyo
kuweza kutatua matatizo yao kwani radio hiyo ipo kwa ajiri yao pia
kudumisha amani na mshikamano baina yao.
Vilevile amelishukuru
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na
Utamaduni- UNESCO kwa kushirikiana na Shirika jingine la Umoja wa
Mataifa la Mpango wa Maendeleo –UNDP, Katika kuhakikisha mradi huo
untekelezwa katika wilaya ya uvinza kama ndoto yake kutetea haki za
akina mama.
Katika uzinduzi huo kumeambatana na mafunzo ya
watangazaji watakao endesha radio hiyo kwa kipindi cha majaribia,
Mkurugenzi huyo amesisitiza wanawke kujitokeza kwa wingi kusaidia kukuza
vipaji vyao na kujikwamua kimaisha kuepukana na mitazamo duni baina yao
kuwa wamesahaulika katika jamii.
Mafunzo hayo yameendeshwa na
Bi ROSE HAJI kwa wanafunzi ishirini kwa wiki moja kwa lengo la
kuwajengea uwezo na jinsi yakutayarisha vipindi kwa mbinu ya UVINZA FM
ikiwa ni mchakato wa kudumisha amani kupitia vyombo vya habari.
MWISHO
Tuesday, June 3, 2014
Tuesday, October 1, 2013
UZINDUZI NRA KATA YA MKONGORO
CHAMA cha National Reconstruction Alliance (NRA)
kimezindua kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Mkongoro
Halmashauri ya wilaya kigoma huku mgombea wake Fadhili Kiswaga akiahidi
kupigania kuboreshwa kwa mazao ya kahawa, nanasi na michikichi ili kuwafanya
wakulima wa mazao hayo kuondokana na umasikini.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa
kampeni hizo uliofanyika kwenye kijiji cha Mkongoro, Mgombea huyo wa NRA alisema
kuwa ni jambo la kusikitiisha kuona kijiji cha Mkongoro kikiwa na sifa kubwa ya
kulima nanasi zinazipendwa huku wakulima wake wako na hali mbaya kwa umasikini.
Alisema kuwa hali hiyo ya wakulima wa mazao hayo
inachangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi waliochaguliwa kushindwa kusimamia
utekelezaji wa miradi ya kuwaondiolea umasikini wananchi na badala yake
viongozi hao kujali maslahi yao.
“ndugu zangu sote tunajua kata ya Mkongoro
inafahamika kwa kilimo cha mazao ya chikichi,kahawa na mananasi lakini wakulima
wa mazao hayo ukiwaangalia wako hoi kwa umasikini, hakuna wa kuwatetea ili kuboreshewa
kwa miundo mbinu ya masoko waweze kuuza mazao yao na kupata faida, Halmashauri
inakusanya kodi kila siku lakini haijali kuweka mazingira mazuri kwa wakulima
hao,”
Nichagueni niwe mtumishi wenu, nikopesheni kura name
nitawalipa maendeleo, nitakuwa kiongozi ambayo atasimama badala ya watu siyo
kama wale walioweka ubinfsi mbele na kunagalia maslahi yao, mmewatuma
halmashauri wakafanyeni kazi lakini wao wanafanya kinyume chake,”alisisitiza
Kiswaga.
Awali mwenyekiti wa chama cha NRA mkoa kigoma,
alisema kuwa chama hicho Khalif Khalfani milembe alisema kuwa chama hicho
kimemsimamisha Kiswaga kwenye uchaguzi huo kutokana na umahiri wake kiutendani
wakiamini kuwa atakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya wananchi wa kata ya Mkongoro.
Milembe alisema kuwa wananchi wa kata hiyo
kutomchagua Kiswaga ni sawa na kuacha dhahabu izolewe na maji na ndiyo maana
chama hicho pia kilimfanya kiongozi huyo kuwa Katibu Mwenezi wake wa Taifa
kutokana na umahiri huo wa utendaji wake.
Akieleza kufanyika kwa uchaguzi huo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya kigoma, Miriam Mbaga alisema kuwa uchaguzi
huo unafanyika kufuatia kifo cha diwani wa kata hiyo, Sospeter Laurent na
kwamba uchaguzi huo utafanyika Februal 9 mwaka huu.
Mbaga alisema kuwa tume ya uchaguzi ilizindua ratiba
ya kampeni Januari 16 mwaka huu hadi Februari 8 ambapo jumla ya vyama saba
vinatareajiwa kushiriki uchaguzi huo vikiwemo CCM, CHADEMA, CUF, NCCR –
Mageuzi, NRA, NLD na DP.
RC KIGOMA AONGOZA MAPOKEZI YA WAZIRI MKUU PINDA
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwapungia wananchi wa mkoa Kigoma waliofika kumpokea kwenye uwanja wa ndege wa Kigoma
Waziri Mkuu mizengo Pinda akipeana mkono na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ambaye alikuwa miongoni mwa mawaziri walioshiriki ziara ya siku sita ya Waziri mkuu Mizengo Pinda mkoani Kigoma
waziri Mkuu Mizengo Pinda akisalimia na mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Agripina Buyogera muda mfupi baada ya waziri Mkuu kuwasili uwanja wa ndege wa kigoma kwa ziara ya kiserikali ya siku sita mkoani humo.
Karibu Kigoma ndiyo anavyoelekea kusema Mkuu wa mkoa Kigoma Kanali Mstaafu, Issa Machibya (kushoto) akimkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeanza ziara ya kiserikali ya siku sita mkoani Kigoma (Picha zote na Fadhili Abdallah)
Waziri Mkuu mizengo Pinda akipeana mkono na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene ambaye alikuwa miongoni mwa mawaziri walioshiriki ziara ya siku sita ya Waziri mkuu Mizengo Pinda mkoani Kigoma
waziri Mkuu Mizengo Pinda akisalimia na mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Agripina Buyogera muda mfupi baada ya waziri Mkuu kuwasili uwanja wa ndege wa kigoma kwa ziara ya kiserikali ya siku sita mkoani humo.
Karibu Kigoma ndiyo anavyoelekea kusema Mkuu wa mkoa Kigoma Kanali Mstaafu, Issa Machibya (kushoto) akimkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeanza ziara ya kiserikali ya siku sita mkoani Kigoma (Picha zote na Fadhili Abdallah)
RC KIGOMA AKIFUNGA MAFUNZO JKT
MKUU wa
mkoa Kigoma Issa Machibya (wa pili kushoto) akikabidhi cheti kwa mmoja
wa vijana waliofanya vizuri katika mafunzi ya JKT kwa vijana wa
kujitolea na wale wa mujibu wa sheria kwenye kambi ya JKT Bulombora
mkoani Kigoma (kulia) ni Mkuu wa kambi hiyo Meja Mohamed Mketo
KUFUNGA MAFUNZO YA JKT
Baadhi ya vijana wanaomaliza mafunzo katika kambi ya JKT Bulombora mkoani kigoma wakipiga kwata kwa kupita kwa mwendo wa haraka mbele ya mkuu wa mkoa kigoma na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe za kufunga mafunzo hayo.
Na Fadhili Abdallah,kigoma
MKUU wa mkoa
Kigoma Issa Machibya amewataka vijana wanaomaliza mafunzo katika kambi za jeshi
la kujenga Taifa mkoani Kigoma kuepuka kujiingiza kwenye matumizi ya madawa ya
kuelvya sambamba na kujiepusha kutumika kuwa wabebaji wa madawa hayo kwani
kufanya hivyo kuna athari kubwa kwa maisha yao.
Akifunga
mafunzo ya vijana wa kujitolea na wale wa mujibu wa sheria yanayojulikana kama Operesheni
miaka 50 ya JKT katika kikosi cha 821
JKT Bulombora wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, Machibya amesema kuwa taifa
linapoteza hazina ya vijana ambao wamekumbwa na wimbi la matumizi na
usafirishaji wa madawa ya kulevya.
Machibya amesema
kuwa vijana ambao wamejitumbukiza katika matumizi ya madawa ya kulevya
wameshindwa kutoa mchango wao katika ujenzi wa taifa na kwamba wengi wao
wanapoanza kutumia madawa hayo hupoteza
uwezo wa kufanya kazi lakini pia kupoteza uwezo wa kufikiri kwa ajili ya maisha
yao.
Kwa upande
wake Mkuu wa kikosi cha 821 JKT Bulombora,Meja Ibrahimu mketo amesema kuwa
vijana 2078 walianza mafunzo hayo ambapo kati yao 150 wameshindwa kumaliza
mafunzo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wengi kudaiwa kuanza mafunzo wakiwa
na mimba ambapo hata hivyo vijana hao pamoja na mafunzo wameweza kutoa mchango
mkubwa kambini hapo ikiwemo shughuli za uzalishaji mali.
Awali katika
risala yao vijana hao iliyosomwa na Maimuna Issa wameomba serikali kuongeza
muda wa mafunzo kwa vijana wanaojiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria
kutoka miezi mitatu ambayo imeanza sasa
na kufikia miezi sita kuwezesha vijana hao kupata mafunzo mengi muhimu ambayo
kwa wakati huu wameyakosa kutokana na muda mfupi waliotumia.
jumla
ya vijana 2078 wamemaliza mafunzo hayo ambapo kati yao vijana wa kujitolea
walikuwa 787 na wale wa mujibu wa sheria
walikuwa 1294.
Mwisho.
Sunday, June 30, 2013
KANISA LA TAG KIGOMA LAWEKWA WAKFU
Askofu Mkuu wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo la Kanisa la TAG Jimbo la Kigoma
Waumini wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiwa wameshika kuta za jengo la kanisa hilo ikiwa ishara ya kuliombea na kuliweka WAKFU.

MAASKOFU, wachungaji na viongozi mbalimbali wa makanisa mkoani Kigoma wakiwa wameshika kuta za kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiliombea na kuliwekea WAKFU kama ishara ya kulizindua rasmi jengo hilo.
Na Mwandishi wetu, Kigoma
ASKAFU Mkuu
wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali amepiga
marufuku viongozi na waumini wa kanisa hilo kutumia nyumba za ibada za kanisa
hilo kuendeshea masuala ya kisiasa.
Mtokambali alisema
hayo alipokuwa akitoa hotuba wakati wa
ufunguzi wa jengo jipya la kanisa la TAG jimbo la Kigoma ambapo askofu huyo
alisema kuwa kama kiongozi mkuu wa TAG hatasita kumfukuza kiongozi au muumini
yeyote ambaye atabainika kutumia majengo ya kanisa kuendesha shughuli za
kisiasa.
Alisema kuwa
kuingiza masuala ya kisiasa katika nyumba za ibada kumekuwa na athari kubwa
katika uendeshaji wa kanisa na kwamba matukio yanayotokea maeneo mbalimbali
nchini ikiwemo kulipuliwa kwa mabomu kwa waumini kanisani msingi wake ni kuacha kuabudu na badala kuendesha siasa.
Aliwaasa
vipongozi na wamumini wa kanisa hilo kwamba nyumba za ibada zinapaswa
kuheshimiwa kama mahali pa takatifu na kudumishwa kama sehemu takatifu ambapo
wenye kukata tama watakimbilia kuokolewa.
Mtokambali
alisema kuwa katika siku za karibuni kumekuwa na matendo mbalimbali ya kisiasa
na uvunjifu wa amani ambapo waumini wa nyumba za ibada wanaendeha maandamano na
kubeba mabango katika kuwakataa viongozi wa madhehebu yao badala ya kutumia vikao
vya kikatiba vya makanisa yao.
Alisema kuwa
TAG imekuwa ikiwafukuza viongozi na waumini wake kutoka katika kanisa hilo kwa
utovu wa nidhamu na kwenda kinyume na maadili ya kanisa kwa sababu suala hilo
lilianza tangu kwa Mungu ambapo shetani alifukuzwa na Mungu baada ya kuasi.
Sambamba na
hilo Askofu huyo ameonya kuwepo kwa vitendo vya ubaguzi, ukabila na unyanyapaa
miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na kwamba vitendo hivyo pia havitavumiliwa
ndani ya kanisa na kuwataka maaskofu na wachungaji kusimamia wajibu wao katika
kusimamia kanisa.
Awali akisoma
risala kwa niaba ya Kanisa hilo mzee wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Alembe
Sadock amesema kuwa jumla ya shilingi milioni 94.7 zimetumika kwa ajili ya
ujenzi wa kanisa hilo kutoka katika mkakati wa kukusanya kiasi cha shilingi
milioni 95.3 na kwamba ili liweze kukamilika kabisa kiasi cha shilingi milioni
55 nyingine zinahitajika kuweza kumalizia ujenzi huo.
Alisema kuwa
sababu ya kanisa kushindwa kukamilika kama ilivyokusudiwa awali ni pamoja na
kupanda kwa gharama za vifaa na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa vifaa
vya ujenzi kutoka maeneo ya nje ya mkoa Dar es salaam.
Kwa upande
wake Mchungaji Kiongozi wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Omari Mlenda amesema
kuwa hadi sasa kanisa hapo lilipofikia hakuna msaada wowote kutoka nje ya nchi
ambao umetumika na kwamba sehemu kubwa ya fedha za ujenzi wa kanisa hilo
zimetoka kwa wauimini wenyewe.
Kwa sasa
mchungaji Mlenda amesema kuwa wauimini na wadau mbalimbali wa kanisa hilo
wanahitaji kujitoa tena kuweza kupata kiasi cha shilingi milioni 55 ambazo
zitatumika kumaliza sehemu ya paa ya kanisa hilo na maeneo machache yaliyobaki.
Mwisho.
WAKULIMA WA KAHAWA KIGOMA WAASWA KUTOKATA TAMAA
Mwenyekiti wa chama kikuu cha wakulima wa tumbaku mkoa kigoma KANYOVU), Mathias Dangwa akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho (kulia) ni Meneja mkuu wa KNYOVU, Jeremia Nkangaza.
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
CHAMA kikuu cha wakulima wa kahawa mkoa kigoma
(KANYOVU) kimewataka wakulima wa mkoa huo
kutokata tamaa na kuanguka kwa bei katika soko la dunia badala yake kuhakikisha
kwamba kahawa inayozalishwa inakuwa na ubora wa juu jambo ambalo ndiyo njia
pekee ya kuwafanya kuwa na soko la uhakika.
Akizungumza
katika mkutano Mkuu wa chama hicho kinachojumuisha vyama vya msingi 11 vya
wakulima wa kahawa mkoani Kigoma Meneja wa Kanyovu Jeremia Nkangaza amesema
kuwa kupanda na kushuka kwa bei kwenye soko la dunia ni jambo la kawaida na
kwamba wakulima wategemee kitu kama hicho kutokea.
Wasi wasi wa
kushuka bei kwa kahawa katika soko la dunia kunafuatia mkakati wa nchi ya
Brazili ambayo ni mzalishaji mkubwa wa kahawa duniani kuongeza uzalishaji hali
ambayo itaathiri bei katika nchi changa zinazozalisha kahawa.
Alisema kuwa
katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya bei katika soko la dunia
mkakati wa chama hicho ni kuhakikisha wanazalisha kwa ubora wa juu na kupata
masoko ya moja kwa moja badala ya kuendelea kupambana katika minada.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Kanyovu, Mathias Dangwa amesema kuwa pamoja na changamoto ya
masoko katika soko la dunia lakini pia amelalamikia kutokuwepo kwa wataalam wa
kahawa kwa ajili ya kutoa maelekezo kwa wakulima katika kusimamia uzalishaji
unaozingatia ubora.
Sambamba na
suala la wataalam Dangwa amesema kuwa upatikanaji wa pembejeo na madawa nalo ni
tatizo na hakuna maelekzo ya moja kwa moja ya kitaalam ya aina ya madawa ya
kutumia na hali hiyo inafanya kila mmoja kutumia madawa ambayo anadhani
anayamudu kulingana na bei.
Kaimu Afisa
kilimo wa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Siwajibu Selemani amekiri kuwepo kwa
wataalam wachache wa kahawa katika halmashauri hiyo lakini mkakati wa serikali
ni kuhakikisha wataalam wanapatikana na kuwafikia wakulima kwa wakati.
Mwisho.
WAJASILIAMALI WATAKIWA KUZINGATIA UBORA KATIKA USINDIKAJI BIDHAA
Mkurugenzi wa udhibiti
ubora wa TBS, Tumaini Mtitu akisisitiza jambo wakati akitoa mada kwenye semina ya wajasiliamali wa mkoa Kigoma
(Picha na Mwandishi wa Habarileo Kigoma)
SHIRIKA la viwango nchini (TBS)
limewataka wajasiliamali wadogo nchini kuzingatia ufungashaji bora wa bidhaa
zao kwani ndiyo pekee inayoweza kuvutia wateja na kupata masoko ya uhakika kwa
ajili ya bidhaa wanazozalisha.
Mkurugenzi wa udhibiti
ubora wa TBS, Tumaini Mtitu amesema hayo kwenye mafunzo kwa wajasilimali wadogo
wa mkoani kigoma kuhusu namna ya kuzingatia usindikaji na ufungashaji
unaozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Mtitu amesema kuwa
pamoja na kuzingatia ubora katika uzalishaji lakini ufungashaji bora wa bidhaa
ni jambo muhimu katika kuvutia wateja bidhaa hiyo inapopelekwa sokoni.
“Wakati mwingine wateja
wanaangalia namna bidhaa zilivyosindikwa kwa maana ya Fainal Product hata kama
hajaona kama uzalishaji wa bidhaa husika imezingatia ubora, kuvutia mteja ni
jambo muhimu sana katika kupata masoko ya bidhaa, na hiyo inatokana na
ufungashaji unaozingatia viwango,”alisema Mtitu.
Akifungua mafunzo hayo
ya siku mbili kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya , Katibu Tawala
msaidi huduma za mipango Geoges Busungu amewataka wajasiliamali wadogo kutumia
elimu wanayopata katika kuboresha shughuli zao.
Busungu alisema kuwa
wajasiliamali wadogo na wa kati ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa eneo
husika lakini wajasiliamali wanapaswa kufanya shughuli zao kwa kufuata
maelekezo ya wataalam wa biashara na hasa suala la uzalishaji linalozingatia
ubora wa viwango na ufungashaji wa bidhaa.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi
ya washiriki wa mafunzo wamesema kuwa yamekuwa na manufaa makubwa kwao kwani
yamewafumbua macho na kupata utaalam wa vitu vingi ambavyo hawakuwa wanavijua
kabla mafunzo hayo.
Hamisi Nkurunzi mmoja wa washiriki
wa mafunzo hayo alisema kuwa ni wazi siku mbili za mafunzo zimekuwa na manufaa
makubwa kwao na zinaweza kubadili na kuboresha utendaji wa shughuli zao ikiwemo
uzalishaji unaozingatia viwango na ufungashaji wake.
Mwisho.
KIGOMA YAONGOZWA KWA AJIRA MBAYA ZA WATOTO
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Imeelezwa kuwa mkoa Kigoma kwa umekuwa ni mkoa
unaoongoza kwa watoto chini ya miaka 18 kutumikishwa katika kazi za ndani nje
ya mkoa huo badala ya kuwa shuleni.
Mtaalam elekezi
uelimishaji jamii wa shirika la uokoaji la kimataifa (IRC), Meshack Petro
alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kupambana na ajira mbaya ya watoto (WEKEZA)
kwenye mashamba ya tumbaku mkoani kigoma
na mashamba ya mkonge mkoani Tanga.
Petro alisema kuwa katika utafiti walioufanya
unaonyesha kuwa hivi sasa watu wengi wamekuwa wakiagiza watumishi wa ndani
kutoka mkoani Kigoma na hivyo kufanya sehemu kubwa ya watoto wa mkoa huo ambao
walipaswa kupata elimu kuokosa.
Ili kukabiliana na tatizo la ajira mbaya kwa watoto
alisema kuwa shirika la IRC kupitia mradi wa WEKEZA inatarajia kuendesha mradi
wa miaka minne wa kupambana na tatizo hilo unaotarajia kugharimu kiasi cha
shilingi bilioni 16.3 kwa ufadhili wa idara ya kazi ya serikali ya Marekani.
Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi wa shirika la IRC,
Elijah Okay alisema kuwa nia ya mradi huo ni kuhakikisha kwamba ajira ya watoto
inatokomezwa kabisa mkoani Kigoma hadi ifikapo mwaka 2016.
Alisema kuwa katika kazi wanazofanyishwa
imegundulika kuwa watoto hao wamekuwa wakifanyiwa unyanyasa mkubwa wa kimwili
na kiakili lakini kubwa ambalo mradi huo unataka kufanya ni kuhakikisha watoto
hao wanarudishwa shuleni na kupatiwa elimu katika watoto wengine sambamba na
mahitaji ya kiuchumi kama kuwawezesha kumudu masomo yao.
Akizindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa
kigoma, Issa machibya Katibu Tawala Msaidizi huduma za uchumi, Michael Orrota
alisema kuwa mkoa Kigoma unakabiliwa na tatizo la watoto wanaotumikishwa katika
kazi mbalimbali ikiwemo mashamba ya tumbaku na kwenye uvuvi.
Orrota alisema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo
kutawezesha kutokomeza mradi huo na kuondoa kabisa tatizo la utumikishwaji wa
watoto lakini pia utawezesha kuinua uchumi wa baadhi ya familia zenye kipato
kidogo ili waweze kuwahudumia watoto wao kupata elimu.
Mwisho.
Katibu Tawala Msaidizi huduma za uchumi Michael Orotta akikata utepe kuashiria uzinduliwa kwa mradi wa kupambana na ajira mbaya za watoto mkoani Kigoma (WEKEZA) anayehuhudia kushoto ni Naibu Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji Ruhonvya Rashidi
(Picha na Fadhili Abdallah)
Subscribe to:
Comments (Atom)











