Sunday, June 30, 2013

KANISA LA TAG KIGOMA LAWEKWA WAKFU

Askofu Mkuu wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa jengo la Kanisa la TAG Jimbo la Kigoma  

 Waumini wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiwa wameshika kuta za jengo la kanisa hilo ikiwa ishara ya kuliombea na kuliweka WAKFU.





MAASKOFU, wachungaji na viongozi mbalimbali wa makanisa mkoani Kigoma wakiwa wameshika kuta za kanisa la TAG jimbo la Kigoma wakiliombea na kuliwekea WAKFU kama ishara ya kulizindua rasmi jengo hilo.
 
 
Na Mwandishi wetu, Kigoma
 
ASKAFU Mkuu wa kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali amepiga marufuku viongozi na waumini wa kanisa hilo kutumia nyumba za ibada za kanisa hilo kuendeshea masuala ya kisiasa.
 
Mtokambali alisema hayo alipokuwa akitoa hotuba  wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la kanisa la TAG jimbo la Kigoma ambapo askofu huyo alisema kuwa kama kiongozi mkuu wa TAG hatasita kumfukuza kiongozi au muumini yeyote ambaye atabainika kutumia majengo ya kanisa kuendesha shughuli za kisiasa.
 
Alisema kuwa kuingiza masuala ya kisiasa katika nyumba za ibada kumekuwa na athari kubwa katika uendeshaji wa kanisa na kwamba matukio yanayotokea maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kulipuliwa kwa mabomu kwa waumini kanisani msingi wake  ni kuacha kuabudu na badala kuendesha siasa.
 
Aliwaasa vipongozi na wamumini wa kanisa hilo kwamba nyumba za ibada zinapaswa kuheshimiwa kama mahali pa takatifu na kudumishwa kama sehemu takatifu ambapo wenye kukata tama watakimbilia kuokolewa.
 
Mtokambali alisema kuwa katika siku za karibuni kumekuwa na matendo mbalimbali ya kisiasa na uvunjifu wa amani ambapo waumini wa nyumba za ibada wanaendeha maandamano na kubeba mabango katika kuwakataa viongozi wa madhehebu yao badala ya kutumia vikao vya kikatiba vya makanisa yao.
 
Alisema kuwa TAG imekuwa ikiwafukuza viongozi na waumini wake kutoka katika kanisa hilo kwa utovu wa nidhamu na kwenda kinyume na maadili ya kanisa kwa sababu suala hilo lilianza tangu kwa Mungu ambapo shetani alifukuzwa na Mungu baada ya kuasi.
 
Sambamba na hilo Askofu huyo ameonya kuwepo kwa vitendo vya ubaguzi, ukabila na unyanyapaa miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na kwamba vitendo hivyo pia havitavumiliwa ndani ya kanisa na kuwataka maaskofu na wachungaji kusimamia wajibu wao katika kusimamia kanisa.
 
Awali akisoma risala kwa niaba ya Kanisa hilo mzee wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Alembe Sadock amesema kuwa jumla ya shilingi milioni 94.7 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo kutoka katika mkakati wa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 95.3 na kwamba ili liweze kukamilika kabisa kiasi cha shilingi milioni 55 nyingine zinahitajika kuweza kumalizia ujenzi huo.
 
Alisema kuwa sababu ya kanisa kushindwa kukamilika kama ilivyokusudiwa awali ni pamoja na kupanda kwa gharama za vifaa na kupanda kwa gharama za usafirishaji wa vifaa vya ujenzi kutoka maeneo ya nje ya mkoa Dar es salaam.
 
Kwa upande wake Mchungaji Kiongozi wa kanisa la TAG jimbo la Kigoma, Omari Mlenda amesema kuwa hadi sasa kanisa hapo lilipofikia hakuna msaada wowote kutoka nje ya nchi ambao umetumika na kwamba sehemu kubwa ya fedha za ujenzi wa kanisa hilo zimetoka kwa wauimini wenyewe.
 
Kwa sasa mchungaji Mlenda amesema kuwa wauimini na wadau mbalimbali wa kanisa hilo wanahitaji kujitoa tena kuweza kupata kiasi cha shilingi milioni 55 ambazo zitatumika kumaliza sehemu ya paa ya kanisa hilo na maeneo machache yaliyobaki.
 
Mwisho.
 

WAKULIMA WA KAHAWA KIGOMA WAASWA KUTOKATA TAMAA




 Mwenyekiti wa chama kikuu cha wakulima wa tumbaku mkoa kigoma KANYOVU), Mathias Dangwa akizungumza katika mkutano mkuu wa chama hicho (kulia) ni Meneja mkuu wa KNYOVU, Jeremia Nkangaza.



Na Mwandishi Wetu, Kigoma

CHAMA  kikuu cha wakulima wa kahawa mkoa kigoma (KANYOVU)  kimewataka wakulima wa mkoa huo kutokata tamaa na kuanguka kwa bei katika soko la dunia badala yake kuhakikisha kwamba kahawa inayozalishwa inakuwa na ubora wa juu jambo ambalo ndiyo njia pekee ya kuwafanya kuwa na soko la uhakika.

Akizungumza katika mkutano Mkuu wa chama hicho kinachojumuisha vyama vya msingi 11 vya wakulima wa kahawa mkoani Kigoma Meneja wa Kanyovu Jeremia Nkangaza amesema kuwa kupanda na kushuka kwa bei kwenye soko la dunia ni jambo la kawaida na kwamba wakulima wategemee kitu kama hicho kutokea.

Wasi wasi wa kushuka bei kwa kahawa katika soko la dunia kunafuatia mkakati wa nchi ya Brazili ambayo ni mzalishaji mkubwa wa kahawa duniani kuongeza uzalishaji hali ambayo itaathiri bei katika nchi changa zinazozalisha kahawa.

Alisema kuwa katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya bei katika soko la dunia mkakati wa chama hicho ni kuhakikisha wanazalisha kwa ubora wa juu na kupata masoko ya moja kwa moja badala ya kuendelea kupambana katika minada.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanyovu, Mathias Dangwa amesema kuwa pamoja na changamoto ya masoko katika soko la dunia lakini pia amelalamikia kutokuwepo kwa wataalam wa kahawa kwa ajili ya kutoa maelekezo kwa wakulima katika kusimamia uzalishaji unaozingatia ubora.

Sambamba na suala la wataalam Dangwa amesema kuwa upatikanaji wa pembejeo na madawa nalo ni tatizo na hakuna maelekzo ya moja kwa moja ya kitaalam ya aina ya madawa ya kutumia na hali hiyo inafanya kila mmoja kutumia madawa ambayo anadhani anayamudu kulingana na bei.

Kaimu Afisa kilimo wa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Siwajibu Selemani amekiri kuwepo kwa wataalam wachache wa kahawa katika halmashauri hiyo lakini mkakati wa serikali ni kuhakikisha wataalam wanapatikana na kuwafikia wakulima kwa wakati.

Mwisho.

WAJASILIAMALI WATAKIWA KUZINGATIA UBORA KATIKA USINDIKAJI BIDHAA



 Baadhi ya wajasiliamali wa mkoani Kigoma wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwsilishwa na maafisa wa Shirika la viwango nchini kwa wajasiliamali hao kuhusu uzalishaji na usindikaji wa bidhaa unaozingatia viwango vya ubora vilivyowekwa.




 Mkurugenzi wa udhibiti ubora wa TBS, Tumaini Mtitu akisisitiza jambo wakati akitoa mada kwenye semina ya wajasiliamali wa mkoa Kigoma
(Picha na Mwandishi wa Habarileo Kigoma)

SHIRIKA la viwango nchini (TBS) limewataka wajasiliamali wadogo nchini kuzingatia ufungashaji bora wa bidhaa zao kwani ndiyo pekee inayoweza kuvutia wateja na kupata masoko ya uhakika kwa ajili ya bidhaa wanazozalisha.


Mkurugenzi wa udhibiti ubora wa TBS, Tumaini Mtitu amesema hayo kwenye mafunzo kwa wajasilimali wadogo wa mkoani kigoma kuhusu namna ya kuzingatia usindikaji na ufungashaji unaozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.


Mtitu amesema kuwa pamoja na kuzingatia ubora katika uzalishaji lakini ufungashaji bora wa bidhaa ni jambo muhimu katika kuvutia wateja bidhaa hiyo inapopelekwa sokoni.



“Wakati mwingine wateja wanaangalia namna bidhaa zilivyosindikwa kwa maana ya Fainal Product hata kama hajaona kama uzalishaji wa bidhaa husika imezingatia ubora, kuvutia mteja ni jambo muhimu sana katika kupata masoko ya bidhaa, na hiyo inatokana na ufungashaji unaozingatia viwango,”alisema Mtitu.



Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili kwa niaba ya  Mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya , Katibu Tawala msaidi huduma za mipango Geoges Busungu amewataka wajasiliamali wadogo kutumia elimu wanayopata katika kuboresha shughuli zao.


Busungu alisema kuwa wajasiliamali wadogo na wa kati ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa eneo husika lakini wajasiliamali wanapaswa kufanya shughuli zao kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa biashara na hasa suala la uzalishaji linalozingatia ubora wa viwango na ufungashaji wa bidhaa.


Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya washiriki wa mafunzo wamesema kuwa yamekuwa na manufaa makubwa kwao kwani yamewafumbua macho na kupata utaalam wa vitu vingi ambavyo hawakuwa wanavijua kabla mafunzo hayo.


Hamisi Nkurunzi mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo alisema kuwa ni wazi siku mbili za mafunzo zimekuwa na manufaa makubwa kwao na zinaweza kubadili na kuboresha utendaji wa shughuli zao ikiwemo uzalishaji unaozingatia viwango na ufungashaji wake.


Mwisho.




KIGOMA YAONGOZWA KWA AJIRA MBAYA ZA WATOTO

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Imeelezwa kuwa mkoa Kigoma kwa umekuwa ni mkoa unaoongoza kwa watoto chini ya miaka 18 kutumikishwa katika kazi za ndani nje ya mkoa huo badala ya kuwa shuleni.

Mtaalam  elekezi uelimishaji jamii wa shirika la uokoaji la kimataifa (IRC), Meshack Petro alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kupambana na ajira mbaya ya watoto (WEKEZA) kwenye  mashamba ya tumbaku mkoani kigoma na mashamba ya mkonge mkoani Tanga.

Petro alisema kuwa katika utafiti walioufanya unaonyesha kuwa hivi sasa watu wengi wamekuwa wakiagiza watumishi wa ndani kutoka mkoani Kigoma na hivyo kufanya sehemu kubwa ya watoto wa mkoa huo ambao walipaswa kupata elimu kuokosa.

Ili kukabiliana na tatizo la ajira mbaya kwa watoto alisema kuwa shirika la IRC kupitia mradi wa WEKEZA inatarajia kuendesha mradi wa miaka minne wa kupambana na tatizo hilo unaotarajia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 16.3 kwa ufadhili wa idara ya kazi ya serikali ya Marekani.

Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi wa shirika la IRC, Elijah Okay alisema kuwa nia ya mradi huo ni kuhakikisha kwamba ajira ya watoto inatokomezwa kabisa mkoani Kigoma hadi ifikapo mwaka 2016.

Alisema kuwa katika kazi wanazofanyishwa imegundulika kuwa watoto hao wamekuwa wakifanyiwa unyanyasa mkubwa wa kimwili na kiakili lakini kubwa ambalo mradi huo unataka kufanya ni kuhakikisha watoto hao wanarudishwa shuleni na kupatiwa elimu katika watoto wengine sambamba na mahitaji ya kiuchumi kama kuwawezesha kumudu masomo yao.

Akizindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa mkoa kigoma, Issa machibya Katibu Tawala Msaidizi huduma za uchumi, Michael Orrota alisema kuwa mkoa Kigoma unakabiliwa na tatizo la watoto wanaotumikishwa katika kazi mbalimbali ikiwemo mashamba ya tumbaku na kwenye uvuvi.

Orrota alisema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutawezesha kutokomeza mradi huo na kuondoa kabisa tatizo la utumikishwaji wa watoto lakini pia utawezesha kuinua uchumi wa baadhi ya familia zenye kipato kidogo ili waweze kuwahudumia watoto wao kupata elimu.

Mwisho.


 Katibu Tawala Msaidizi huduma za uchumi Michael Orotta akikata utepe kuashiria uzinduliwa kwa mradi wa kupambana na ajira mbaya za watoto mkoani Kigoma (WEKEZA) anayehuhudia kushoto ni Naibu Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji Ruhonvya Rashidi 
(Picha na Fadhili Abdallah)

Sunday, May 19, 2013

KIKAO CHA MAHAKAMA KUU KIGOMA

 Jaji wa mahakama kuu kanda ya Tabora Sam Mpaya Rumanyika akikagua gwaride la askari wa kikosi cha kutulia ghasia ikiwa ishara ya kuanza kwa kikao cha mahakama kuu mkoani Kigoma


Jaji wa mahakama kuu kanda ya Tabora Sam Mpaya Rumanyika akipokea salamu za utii kutoka kwa kikosi cha askari wakutuliza ghasia (Hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kikao cha mahakama kuu kanda ya Tabora mkoani Kigoma (kulia) ni Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser Kashai na nyuma ni watumishi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa mkoa kigoma Issa machibya

WADAU WA HABARI KIGOMA

 Wadau wa habari mkoani Kigoma wakifuiatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolwa siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma.


Kamanda wa polisi Fraisser Kashai ambaye alikuwa mgeni rasmi siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma akitoa hotuba yake kwa washiriki wa maadhimisho hayo

SIKU YA UHURU WA HABARI NCHINI

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Kigoma Deo Nsokolo (kushoto) akizungumza katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani aliyekaa kati kati Ni Kamanda wa polisi mkoa kigoma Fraisser Kashai aliyekuwa mgeni rasmi na kulia Afisa habari ofisi ya mkuu wa mkoa kigoma, Edward Ng'onoli


Wadau wa habari mkoani Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni Rasmi Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser Kashai siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma
 
Waandishi wa habari kutoka chama cha waandishi wa habari mkoani Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja na kamanda wa polisi mkoa Kigoma Fraisser kashai mwenye kofia waliokaa wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma (Picha zote na Fadhili Abdallah)

 
Na Mwandishi wetu, Kigoma
 
WAANDISHI wa habari mkoani Kigoma wametakiwa kutumia  kalamu zao kwa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari kwani zikitumika vizuri zinaweza kuwa chachu na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya jamii na kwamba kinyume chake kalamu za waandishi zinaweza kugeuka risasi na kuleta maafa makubwa kwa jamii.

Diwani wa kata ya Mwanga Kaskazini, Francis Mangapi alisema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani Kigoma yaliyoratibiwa na chama cha waandishi wa habari mkoani humo (KGPC).

Mangapi alisema kuwa tumeshuhudia maeneo mbalimbali ambapo waandishi wametumika vizuri kumekuwa na maendeleo makubwa na jamii imehamasika katika kujieleta maendeleo lakini mahala ambapo waandishi wametumika vibaya kumekuwa na matatizo makubwa makubwa.

Akichangia kuhusiana na jambo hilo Mfanyabiashara maaruru wa mjini Kigoma Miforo Mpozemenya alisema kuwa waandishi wa habari wasikubali kutumiwa na wanasiasa ama makundi mbalimbali kwa faida zao badala  yake wajikite katika kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya jamii na kufuata maadili ya taaluma yao.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Fraisser Kashai ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo baina ya waandishi na jeshi lake lakini waandishi wa habari wamekuwa mchango mkubwa katika kufanikisha mambo mbalimbali ya kiutendaji ndani ya jeshi la polisi.

Kashai alisema kuwa jeshi lake litaendelea kutoa msaada na kushirikiana na vyombo vya habari kwa kadri iwezekanavyo na kwamba kama kuna kutoelewana mahali baina yao ofisi yake iko wazi muda wote kwa ajili ya majadiliano na kuzungumza namna gani ya kuweza kufanya kazi pamoja.

Awali Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa kigoma, Deogratius Nsokolo, matukio ya hivi karibuni ya kuuawa kwa mwandishi wa habari,Daudi Mwangosi wa Iringa, Issa Ngumba wa Kibondo mkoani Kigoma na kuteswa na kutobolewa jicho kwa Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri Tanzania, Absolom Kibanda kunawafanya waandishi wa habari watafakari namna ya utekelezaji wa majukumu yao.

Hata hivyo Nsokolo alisema kuwa matukio hayo badala ya kuwarudisha nyuma na kuwavunja moyo badala yake vimewapa ari , ujasiri na mbinu mpya waandishi wa habari    katika kuendeleza majukumu yao lakini pia kufichua mambo mabaya ambayo yanafanywa na watu wachache huku mambo hayo ikiacha jamii kubwa ya Watanzania ikiteseka.

Mwisho.

WANAOHAMISHWA KIBIRIZI WALALAMIKIA FIDIA KUCHELEWA


Na Fadhili Abdallah,Kigoma


wafanyabiashara na wananchi waliokuwa wakiishi na kufanya shughuli zao katika eneo la bandari ndogo ya kibirizi Manispaa ya kigoma ujiji, wamelalamikia hatua ya manispaa hiyo kuchelewesha kuwalipa malipo yao ya fidia na kuwazuia kufanya shughuli zozote za kujiingizia kipato.


Wakizungumza katika mahojiano maalum na gazeti  wananchi hao wamesema kuwa baada ya kufanywa tathmini ya upanuzi wa bandari ndogo ya Kibirizi manispaa ya Kigopma Ujiji zaidi ya mwaka mmoja uliopita   lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika.


Mmoja wa wananchi hao Patrick Ntahondi alisema kuwa amekuwa na hali ngumu kimaisha kwani hawezi kufanya lolote katika eneo lake kwa sasa kwa sababu watu wengi wameshahama na kuhamisha shughuli zao lakini wao hawaelewi mambo yakoje na kuwawia ngumu kuendesha maisha yao.


Naye Jasmine Katekwe alisema kuwa ana nyumba yake katika eneo hilo ambayo alikuwa akiitumia kupangisha wafanyabishara kuhifadhi mizigo yao na pia kuwapa eneo la kukaushia samaki na dagaa lakini serikali imesimamisha shughuli za biashara na hali kiuchumi kwake imekuwa ngumu.


Sambamba na hilo alisema kuwa anashindwa kufanya marekebisho yeyote katiuka nyumba yake kutokana na serikali kueleza kwamba tayari tathmini imeshafanyika ambapo wameiomba serikali kuingilia kati na kuwaruhusu waendelee na shughuli za kuwaingizia kipato na makazi.



Akizungumzia jambo hilo Naibu Meya wa Manispaa ya Kigoma Rashidi Ruhonvya  amesema kuwa kuchelewa kulipwa fidia kwa wananchi wa eneo hilo kumetokana na kukosewa kwa tathmini ya awali baada ya kuwepo kwa baadhi ya wananchi ambao hawakujumuishwa licha ya maeneo na vibanda vyao kubainishwa.

Alisema kuwa tayari muhakiki ameshafika na anaipitia upya repoti ya tathmini kuona kama kuna itilafu mahali na kwamba baada ya kufanyiwa marekebisho kwa itililafu zilizojitokeza malipo ya watu hao yatafanywa haraka iwezekanavyo na kwani uhakiki huo umefikia hatua ya mwisho.


Hata hivyo Ruhovya ametoa wito kwa watu wote waliokuwa wakiishi na kufanya shughuli mbalimbali katika eneo hilo kusitisha mambo hayo wasubiri kulipwa fidia zao na kutafuta maeneo mengine kwa ajili ya makazi na shughuli zao.

Mwisho.


ILI kuhakikisha wanawatumia watoto wao katika shughuli zao za kiuchumi badala ya kuwa shuleni imebainika kuwa wazazi wengi katika vijiji mbalimbali vya  wilayani Kibondo  wanakaidi kwa makusudi kuwalipia ada na michango mbalimbali watoto waliofaulu na kuchaguliwa  kujiunga na masomo ya sekondari wilayani humo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti na kuthibitishwa na ngazi mbalimbali za uongozi wa kiserikali na kijamii imethibitisha kwamba  vitendo hivyo vimefanya uongozi wa shule za sekondari katika wilaya hiyo na serikali za vijiji na kata kutumia muda mrefu katika kuhangaika kuwaokoa watoto hao na vitendo vya wazazi wao.

Akithibitisha kuhusiana na hilo Mkuu wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kumgogo tarafa ya Mabamba wilayani humo, Adolf Tuseko alisema kuwa vitendo vya wazazi kukaidi kuwalipia ada watoto kwa makusudi vimechukua nafasi kubwa ya shughuli za utawala shuleni hapo zaidi ya shughuli za kitaaluma.

Mkuu huyo wa shule alithibitisha kwamba wazazi wanatumia hila ya kutokuwa na fedha za kuwalipia watoto wao ili watoto hao watakaporudishwa nyumbani iwe rahisi kwao kuwatumia kwa shughuli za kufanya vibarua kwenye mashamba na biashara kwenye magulioa.

Alisema kuwa kufuatia hali hiyo wanalazimika kulipeleka suala hilo katika uongozi wa kata ambapo majina ya wazazi ambao wanachukua muda mrefu kutolipa michango hiyo hupelekwa huko na mtendaji wa kata na baraza la maendeleo la kata ndiyo husimamia hilo.

Akizungumzia kuhusiana na hilo Mwalim Mkuu wa shule ya Msingi Mkarazi, Asumwisye Peter alisema kuwa  pamoja na madai ya kipato kidogo cha wazazi lakini wazazi wengi hawana mwamko wa elimu na ndiyo maana hawaoni umuhimu wa watoto wao kuendelea na masomo ya sekondari.

Alisema kuwa kabla ya ujenzi wa sekondari za kata watoto wengi walikuwa wakiishia darasa la saba na wazazi walikuwa wakipata nafasi ya kuwatumia watakavyo na kuwafanya ndiyo chanzo cha kuingiza mapato kwa ajili ya kuendesha familia kutokana na kutumika kwenye kufanya kazi za vibarua.

Anasema kuwa wakati mwingine hasa wakati wa magulio au wakati wa kilimo watoto wengi hutolewa shuleni na kwenda kufanya kazi kwenye mashamba au masoko na hiyo si kwa shule za msingi tu bali hata kwa shule za sekondari na imekuwa ni tatizo kubwa kati ya shule na jamii inayozunguka shule hizo ambao watoto wao wanasoma hapo.

Kwa upande wake mmoja wa wazazi walioongea na gazeti hili, Method Kalumanzila alithibitisha kwamba kitendo cha wazazi kutolipa ada na pia kuwatoa watoto shule kwa ajili ya kwenda kufanya vibarua imekuwa tatizo sugu na kikubwa ni mwamko mdogo wa wazazi katika elimu na hali duni ya kipato kwa wazazi.

Naye Mzazi mwingine, Magreth Sunzu mfanyabiashara katika soko la Mabamba alisema kuwa  wazazi hawaoni umuhimu wa watoto wao kuendelea na masomo ya sekondari kwa sababu baada ya miaka minne ya masomo wengi huambilia alama sifuri (Division Zero) na kubaki nyumbani kama wenzao walioishia darasa la saba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kigoma, Leopold  Ulaya alithibitisha matatizo hayo mawili kuikabili wilaya yake na kusema kuwa wamo katika mchakato wakuona wafanye nini kukabiliana na hali hiyo lakini kwa sasa uongozi wa kata umepewa mamlaka ya kuwachukulia hatua wazazi kwa kuwafikisha kwenye baraza la kata na kuwatoza faini.

Sambamba na hilo alisema kuwa wanatarajia kutembelea halmashauri ambazo zinachamoto kama ya kwao ili kuona namna gani wanafanya kukabiliana na hali hiyo lakini pia wanawaza namna ya kutunga sheria ndogo za halmashauri ambazo zitawabana na kuhakikisha kwamba wanalipa michango ya watoto wao na pia kuhakikisha kwamba watoto wao kuhudhuria masomo.

Mkuu wa wilaya kibondo kwa upande wake alisema kuwa utoro kwa wanafunzi wa sekondari kuacha masomo na kwenda kufanya shughuli za biashara na vibarua ni tatizo kubwa lakini pia suala la wazazi kukataa kulipia gharama za masomo ya watoto wao ni tatizo lingine ambayo kwa pamoja wanayatarajia kuyafanyia kazi katika kikao cha wadau wa elimu wanachotarajia kuitisha.

Mwisho.